
Sweetbert Lukong | CHAMPIONI | Dar es Salaam
WAKATI Simba ikiwa katika harakati kabambe za kuhakikisha msimu huu inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la FA, huenda timu hiyo ikampoteza kiungo wake Mohamed Ibrahimu ‘MO’.
MO ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, hivi sasa anawindwa kila mahali.
Meneja wa kiungo huyo, Jamal Kisongo ameliambia Championi Jumatano kuwa, tangu mchezaji huyo atue Simba amekuwa akipata ofa mbalimbali kutoka nje ya nchi kutokana na kuvutiwa na kiwango chake.
Kutokana na hali hiyo, Kisongo alisema endapo mambo yatakuwa mazuri basi mchezaji huyo anaweza kuondoka Simba baada ya kumalizika kwa msimu huu.
“Kwa sasa Mo hawezi kuondoka Simba kwa sababu bado timu yake hiyo inamhitaji katika harakati zake za kuwania ubingwa wa ligi kuu.
“Hata hivyo, baada ya ligi kumalizika hapo ndipo tutakapoangalia sasa kama anaweza kuondoka na kwenda kujaribu bahati yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchini, kwani tayari ameshapata uzoefu na kuna ofa nyingi.
“Lakini kabla ya mambo yote itabidi tuwasiliane kwanza na Simba ambao ndiyo wanaomiliki kwa sababu bado ana mkataba nao,” alisema Kisongo.