
GABRIEL NG’OSHA GAZETI LA AMANI, HABARI
MWANZA: Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini, amevitaka vituo vya runinga na redio nchini kuacha kusoma habari kamili za magazetini na kuvitaka vyombo hivyo kusoma habari kwa ufupi ili kuwavutia wanunuzi wa magazeti.
Katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yalifanyika jijini Mwanza, Dk. Mwakyembe alielekeza kuwa, kusoma habari zote za magazetini kwenye runinga na redio ni kuharibu biashara ya magazeti hivyo vyombo hivyo viwe vinasoma habari kwa ufupi tu.
Dk. Mwakyembe alisema ataendelea kutetea na kulinda haki za waandishi wa habari huku akiwahakikishia ulinzi waandishi wa habari za uchunguzi na kuongeza kuwa kuwepo na ushirikiano wa kutosha kwa wamiliki wa vyombo vya habari na kuagiza Idara ya Habari (Maelezo) kutengeneza mawasiliano ya kudumu na kukutana angalau mara moja kwa mwezi, kujadili udhaifu unaojitokeza na kuchukua hatua stahiki.