Wilbert Molandi na Ibrahim Mussa | CHAMPIONI | DAR ES SALAAM
ISHU ya Mohammed Fakhi, juzi Yanga waliikumbuka na kukwepa mtego wa kupokwa pointi tatu, baada ya kushtuka na kumtoa kwenye kikosi cha kwanza kipa wake, Deogratius Munishi ‘Dida’ dakika chache kabla ya mpira kuanza.
Dida alitolewa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kilichocheza na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Beki wa Kagera, Fakhi hivi karibuni aliisababishia timu kupokwa pointi tatu na Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kupewa Simba waliopokwa baadaye na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho hilo.
Juzi, Dida alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotakiwa kucheza katika mchezo huo lakini alilazimika kuondolewa muda mfupi kabla ya kuingia uwanjani kufanya mazoezi mepesi.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kipa huyo walimtoa dakika chache wakati timu zinaingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli na nafasi yake kuchukuliwa na Beno Kakolanya.
Saleh alisema, wakati wanajiandaa kuingia uwanjani, walipigiwa simu na viongozi na kuulizwa kutaka kujua idadi ya kadi za njano ambazo anazo Dida ambazo waliziangalia na kubaini ana mbili pekee.
Alisema ilibidi ajiridhishe tena kwa kocha wa viungo wa timu hiyo Mzambia, Noel Mwandila ambaye naye anatunza kumbukumbu za kadi na kujiridhisha hana kadi tatu kama ilivyoelezwa.
Aliongeza kuwa, licha ya kujiridhisha hakuwa na kadi tatu za njano lakini yeye kwa kushirikiana na Kocha Mkuu, George Lwandamina waliamua kumuondoa na kumchezesha Kakolanya ili kuwa salama.
“Dida tulimtoa kikosini kwa hofu baadaye kutokea yaliyotokea kwa beki wa Kagera, Fakhi ambaye alidaiwa kucheza mechi na Simba akiwa na kadi tatu za njano huku taarifa nyingine zikisema zilikuwa ni kadi mbili pekee.
“Tuliona tumuondoe kikosini kwa tahadhari na kumuita Barthez ‘Ally Mustapha’ aliyekuwa nyumbani kufanya haraka awahi uwanjani kwa ajili ya kukaa benchi la wachezaji wa akiba.
“Jambo la kushukuru tulifanikiwa kuukwepa mtego huo na baada ya Barthez kufika haraka tulimpeleka kwa kamishna wa mchezo kwa ajili ya kukaguliwa na kuingizwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba,” alisema Saleh.