
Said Ally na Omary Mdose | CHAMPIONI| DAR ES SALAAM
UHAKIKA wa kiungo wa Yanga, Simon Msuva kubakia ndani ya timu hiyo kwa ajili ya kuichezea kwa msimu ujao unazidi kuwa mdogo baada ya klabu mbili kutoka Falme za Kiarabu (U.A.E) kuweka wazi nia ya kumtaka kiungo huyo.
Msuva mwenye mabao 12 kwenye Ligi Kuu Bara, amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kukitumikia kikosi hicho ambacho kinanolewa na Mzambia, George Lwandamina.
Meneja wa kiungo huyo, Jonas Tiboroha, ameliambia Championi Jumatatu, kuwa klabu zinazomtaka kiungo huyo ni Al Masry pamoja na Etihad ambazo zinahitaji kwa hali na mali saini ya kiungo huyo ambaye amekuwa na msimu mzuri ndani ya kikosi hicho.
“Ni kweli timu hizo za Uarabuni zimeonyesha nia ya dhati ya kumtaka Msuva baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu ambapo wamekoshwa na kiwango chake ambacho anakionyesha kila siku ambapo pia tumewatumia video zake ambazo ameitumikia timu hiyo.
“Kilichobaki kwa sasa ni Yanga wenyewe waweke wazi juu ya kiasi gani cha fedha ambacho wanakihitaji kwa ajili ya kumuachia kiungo huyo na naamini kwamba kila kitu kitakwenda vizuri endapo wao watakubali juu ya dili la mchezaji huyo kwenda kutumika nje ya nchi,” alisema Tiboroha.
Ukiwaondoa Waarabu hao pia kiungo huyo ameshawahi kutakiwa na timu ya Zanaco ya Zambia ambayo ilivutiwa na kiwango chake baada ya kukutana kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa upande wake Msuva amesema: “Mimi bado nina mkataba na Yanga, hivyo timu yoyote inapokuja kunitaka lazima iwasiliane na viongozi wangu ambao wenyewe ndiyo watajua kwamba waongee nao au vipi lakini kama mambo yakiwa sawa nitaenda kujiunga nao kwani natamani kucheza soka nje ya nchi.”
Championi Jumatatu lilipomtafuta Katibu wa Yanga, Boniface Mkwasa kuzungumzia ishi huyo alisema: “Kweli tumepokea barua za timu hizo zinazomtaka Msuva lakini tatizo kubwa lililopo ni kwamba zina hitilafu ya kuonyesha zinaenda kwa nani (mfano mwenyekiti, katibu na kadhalika).”