×

Mkali wa Mabao Ligi Kuu Aziita Simba, Yanga

Ibrahim Mussa|GPL

KINARA wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara, Abdulrahman Mussa, ameziita timu za Yanga na Simba kuweza kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu kwa kuwa mkataba wake na Ruvu Shooting unafikia tamati mwishoni mwa msimu hu.

Abdulrahman anaongoza katika mbio za ufungaji bora akiwa na mabao 12 sawa na Simon Msuva wa Yanga wakiwa wanafukuzana katika kuwania kukitwaa kiatu cha dhahabu msimu huu.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Abdulrahman alisema kuwa, mkataba wake Ruvu Shooting unakaribia kuisha mwishoni mwa msimu huu, hivyo yupo tayari kutua katika timu yoyote itakayomhitaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu kwa dau ambalo watakubaliana.

Nimefurahi kuona nimefanikiwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huu, hii imetokana na juhudi ambazo nimekuwa nikizifanya tangu mwanzo hadi kufikia hapa nilipo kwa kufukuzana na wakongwe Msuva na Shiza Kichuya, naamini Mungu atajalia niweze kutwaa kiatu hicho.

Kwa sasa mimi nakaribia kumaliza mkataba wangu na Ruvu mwishoni mwa msimu huu, hivyo nipo tayari kwenda timu yoyote ile itakayonihitaji zikiwemo Simba na Yanga, nazikaribisha na nipo tayari kutua kokote kule, ila kuhusu suala la dau hadi nitakapokutana na timu husika ndiyo nitaweka wazi kiasi nitakachokihitaji.

Kwa sasa hakuna timu iliyonifuata, lakini nitakuwa tayari kuondoka Ruvu iwapo nitapata ofa,” alisema Abdulrahman.

Alimalizia kwa kusema kuwa, siri ya mafanikio ya kiwango chake ni kocha Boniface Mkwasa ambaye ndiye aliyemjenga tangu akiwa katika kikosi B cha timu hiyo kipindi anakinoa kikosi hicho.

 

Leave a Comment