
DROO ndogo ya nne ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imewadia na sasa itafanyika Mei 31, mwaka huu na kama kawaida washindi watapata zawadi mbalimbali ikiwemo ile kubwa ya pikipiki.

Afisa Masoko wa Kampuni ya Global Publishers, inayoendesha bahati nasibu hiyo, Yohana Mkanda alisema kuwa baada ya kufanya droo tatu ndogo kwa mafanikio makubwa, sasa inakuja ya nne ambayo itafanyika mwishoni mwa mwezi huu katika eneo ambalo bado linafanyiwa kazi.

“Tuna uhakika wa kufanya droo hiyo mwisho wa mwezi huu, lakini kuhusu wapi tutalifanyia zoezi hilo, bado tunaendelea na mazungumzo na mara itakapokamilika, tutawafahamisha wasomaji wetu ili wajiandae kwa shughuli hiyo.

“Kama wanavyojua tumeanza kuboresha zawadi zetu kwa kadiri tunavyokwenda, katika droo zetu tatu ndogo ambazo tumeshazifanya, jumla ya pikipiki tatu zimeshatolewa, televisheni kubwa flat screen tatu pia, dinner set tatu na simu za kisasa nyingi tu.
“Tunawasihi waendelee kusoma magazeti yetu ambayo licha ya bahati nasibu hiyo, pia yanawaletea habari motomoto za kijamii, michezo, burudani na mastaa mbalimbali.

“Katika magazeti yetu yote, kwenye kurasa za pili zipo kuponi zenye maelekezo ya namna ya kufanya, wakishamaliza kujaza, wanaweza kuzituma kwetu kupitia kwa mawakala wetu waliopo nchi nzima na wale wa Dar es Salaam wanaweza kuja ofisini kwetu, Bamaga Mwenge na kuziacha kwenye ndoo ya kukusanyia kuponi,” alisema Mkanda.
Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imedhaminiwa na Kampuni ya Tecno Mobile, King’amuzi cha Ting, British School na Kilimanjaro Institute of Technology.