
Na Said Ally|CHAMPIONI|GPL
TAYARI Simba imeanza kujipanga kwa ajili ya michuano ya kimataifa kwa msimu ujao kwani hivi sasa tunavyoongea imemficha katika moja ya hoteli za kifahari jijini Dar, beki wa kati anayetajwa kuvaa viatu vya Mganda, Juuko Murshid.
Simba ambayo kwa takriban misimu minne haikushiriki michuano ya kimataifa, msimu ujao itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ili kukiimarisha kikosi chake, imempa mkataba wa miaka miwili aliyekuwa beki wa kati wa Toto Africans ya Mwanza, Yusuph Mlipili.
Baada ya Mlipili kusaini Simba, vigogo wa klabu hiyo wakaamua kumficha katika Hoteli ya Saphire iliyopo Kariakoo jijini Dar ambapo kikosi kizima cha timu hiyo ndipo kimeweka kambi hapo kikijiandaa na michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kuanza leo Jumatatu.
Mlipili ameliambia Championi Jumatatu, kuwa baada ya kusaini katika kikosi hicho kwa kazi kubwa iliyobakia ni kwake kuwathibitishia viongozi hao uwezo wake kwa kuonyesha uwezo mkubwa.
“Kweli nimesaini Simba kwa miaka miwili na sasa nipo na wachezaji wengine kwa ajili ya kujiwinda na SportPesa Super Cup ambapo huko nitaanza kuonyesha uwezo wangu.
“Najua kuna ushindani mkubwa hapa lakini kwangu sihofii lolote lile kwa sababu ninajiamini na najua nitacheza katika kikosi cha kwanza kwa sababu nina uwezo kama walionao mabeki wengine wa hapa,” alisema Mlipili.