×

Bodaboda Ajigongesha Makusudi Kwenye Nguzo Akiwa Amembeba Askari, Afariki

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limelazimika kutumia mabomu kuwatawanya madereva bodaboda zaidi ya 100 waliokuwa wanaandamana kuelekea eneo la Ibinzamata kwenye msibani kwa dereva mwenzao, Joel Mamla (26), ambaye alifariki dunia Juni 6, 2017 akiwa amempakia askari wa usalama barabarani aliyekuwa amemkamata kwa kosa la kutovaa kofia ngumu (helmet).

Joel ambaye alikamatwa na askari waliokuwa kwenye majukumu yao ya kila siku, aliamuliwa kuelekea kituo cha polisi huku akiwa na askari amembeba kwenye pikipiki yake lakini baadaye anadaiwa kuwa alibadilisha uelekeo na kwenda Barabara ya Tinde huku akimwambia askari watakufa pamoja kisha kuigongesha pikipiki kwenye nguzo ya alama za barabarani na baadaye kufariki dunia huku askari huyo akijeruhiwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Jumanne Murilo, amekiri kutokea kwa tukio hilo.

“Dereva bodaboda huyo baada ya kukamatwa aliamriwa kuelekea kituoni, ndipo akambemba askari PC Edmond, lakini kabla hawajafika kituoni, ghafla alielekeza pikipiki mahali pengine huku akimwambia askari lazima wafe wote.

 

“Wakati pikipiki hiyo ikiwa kwenye mwendo kasi, askari huyo alianza kujihami kumzuia lakini bahati mbaya hakufanikiwa na hatimaye kutokea ajali hiyo iliyosababisha kifo cha dereva huyo,” alisema Kamanda Murilo.

Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo, wananchi kwa kushirikiana na bodaboda walianzisha vurugu kwa kuwarushia mawe polisi, ndipo jeshi hilo lilipotumia nguvu ya ziada kupiga mabomu, ili kuimarisha usalama na hali ya amani ambapo hatimaye waliidhibiti hali hiyo.

Na:Gabriel Ng’osha/GPL

Leave a Comment