
Madrid, Hispania | Championi Jumatano | Makala
PAMOJA na kwamba Cristiano Ronaldo alipewa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya walipovaana na Juventus na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, lakini ni kosa kubwa kama watu hawataheshimu kiwango cha kiungo wa timu hiyo, Isco. Kiungo huyo ambaye alikuwa kwenye hatihati ya kucheza mchezo wa fainali, hakika alifanikiwa kuonyesha kiwango cha juu sana na kuipa timu yake ushindi huo muhimu.
Isco ambaye awali alikuwa anatajwa kuwa anaweza kuondoka kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu huu, alishika nafasi ya pili kwa ubora nyuma ya Ronaldo na kuzidi kuonyesha kuwa hakukuwa na upendeleo wowote kwa yeye kucheza mchezo huo kama wengi walivyokuwa wakifikiri. Iliaminika kuwa Gareth Bale, alikuwa anatakiwa kuanza kwenye mechi hiyo, lakini baadaye kocha wa Real, Zinedine Zidane, akaamua kumuanzisha Isco ambaye alifanya kazi kubwa kuliko wengi walivyokuwa wakifikiria.

Kiungo huyo ambaye ameonyesha kiwango cha juu sana msimu huu, amefanikiwa kucheza jumla ya michezo 42 na kufunga mabao 11 na amekuwa akitajwa kuwa anawindwa na timu kadhaa kubwa ikiwemo Manchester United, Liverpool na Manchester City, lakini mwenyewe amefungua mdomo wake kwa kusema hana mpango wa kuondoka Real kwa kuwa ameona ndiyo klabu bora kwake. “Real ni timu kubwa duniani, hakuna anayeweza kukataa hilo, hii ni timu bora Madrid ambayo imeweka rekodi ya kutwaa makombe makubwa kadhaa.
“Sioni sababu yoyote inayoweza kunifanya niondoke hapa, hapa ni kama nyumbani na nataka kuona nasaini mkataba mpya. “Hii ni klabu bora na yenye heshima kwa kila mmoja ambaye amekuwa akiitumikia, nitazungumza na uongozi baadaye nijue nini kitafuata, lakini ninaaminikuwa nipo nyumbani,” anasema Isco mwenye umri wa miaka 25. Taarifa zimekuwa zikisema kuwa, Zidane alizungumza na kiungo huyo juzi na kuna uwezekano mkubwa akapewa mkataba wa miaka mitano wa kuendelea kuitumikia timu hiyo. “Hatuna haraka sana na wachezaji wetu, tunaamini kuwa kila mmoja ana mapenzi ya dhati kwenye timu hii na wanaweza kukubali kusaini mikataba mipya nasi kwa kuwa hii ni kati ya timu bora duniani.

“Ingawa tutazungumza na kila mmoja na kumpa heshima yake anayostahili, kila aliyetutumikia akiwemo Isco na wengine, tutamweka kwenye kundi moja na kumpa heshima ya kutosha,” anasema Zidane. Mkataba wa Isco umebakiza mwaka mmoja na kuna hofu kuwa kuendelea kukaa bila kuongezewa mkataba kunaweza kumfanya akaanza mazungumzo na baadhi ya klabu nyingine.

Akiwa na umri mdogo, kiungo huyo anaweza kujiunga na timu nyingine yoyote kubwa kwa kuwa tayari ana hazina kubwa ya makombe. Ameshatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu akiwa na Real Madrid pamoja na ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, akiwa na timu hiyo hiyo msimu huu. “Huu ni ubingwa wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Madrid baada ya kipindi cha miaka minne. “Kwangu natwaa ubingwa huu kwa mara ya tatu kama mwanasoka wa kulipwa, sikuwa nafikiri kuhusu hilo lakini napenda kuishukuru familia yangu ambayo imefanya kila kitu hapa kuwa rahisi,” anasema kiungo huyo mwenye pasi zenye macho.
Isco ameshaitumikia Real kwenye michezo 191 na kufunga mabao 33, tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2013 akitokea Malaga ambayo alikuwa ameichezea michezo 47 na kufunga mabao 12. Ni kati ya wachezaji wenyewe umri mdogo ambao wametwaa makombe mengi akiwa ameshachukua makombe nane makubwa tangu alipoanza kucheza soka la ushindani mwaka 2011 akiwa na Valencia. Ameshatumika kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kwenye michezo 19 na kufunga mabao matatu.