
Na Richard Bukos
DAR ES SALAAM: Washindi wa droo ndogo ya 4 wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya pili, iliyochezeshwa wiki iliyopita kwenye Viwanja vya CCM Mwinjuma, Mwananyamala jijini. Leo Jumatatu ilikuwa ni siku yao ya furaha tele baada ya kukabidhiwa zawadi zao kwenye hafla iliyofanyika ofisi za Global Publishers zilizopo Bamaga Mwenge.

Washindi hao wamekabidhiwa zawadi hizo baada ya kujishindia Bahati Nasibu hiyo inayoendeshwa na Kampuni ya Global kwa usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Body) kwa kununua magazeti ya kampuni hiyo na kukata kipande cha kuponi kilichopo kwenye magazeti hayo.

Magazeti hayo ni Uwazi, Ijumaa, Amani, Risasi Jumatano, Risasi Jumamosi, Ijumaa Wikienda na Championi ambayo yote yana kuponi ya kushiriki shindano hilo.

Katika hafla hiyo aliyeanza kukabidhiwa zawadi yake ni Peter Christopher Katua wa Ilala jijini Dar, ambaye alijishindia seti ya vyombo (dinner set).

Mshindi huyo baada ya kukabidhiwa zawadi yake alisema anaishukuru Global kwa kuendesha Bahati Nasibu hiyo ambayo inawanufaisha wasomaji wa magazeti yake.

“Ukweli nimefarijika sana na zawadi hii kwakuwa sikutegemea kama ningeweza kuibuka mshindi, yaani nilikuwa kama nabahatisha lakini nimeibuka mshindi wa hii dinner seti kwa kuponi moja ya gazeti nililolinunua shilingi mia tano tu. Ukweli imenipa raha sana”. Alimaliza kusema Peter.

Aliyefuatia ni Nuhu Halifa Kachenje ambaye alifika kwenye hafla hiyo kwa ajili ya kumpokelea zawadi ya simu ya kisasa ‘smart phone’ ndugu yake, Ally Halifa Kachenje ambaye hakuweza kufika wakati wa makabidhiano hayo.

Baada ya wawili hao kukabidhiwa vyao funga kazi ilikuwa kwa mshindi wa zawadi ya tatu, Shabani Ahmadi Ngao wa Tabata Dar aliyeibuka mshindi wa pikipiki.

Ngao alifika kwenye hafla hiyo akiwa na mkewe Leyla Alex ambapo alisema mwanamke huyo ndiye chanzo cha ushindi huo kwakuwa ndiye aliyemuhamasisha kushiriki Bahati Nasibu hii.

“Mimi ni msomaji mzuri wa magazeti ya Global kwa kipindi kirefu lakini awali nilikuwa nasoma bila kujaza kuponi lakini huyu mke wangu ndiye aliyenihamasisha kukata kuponi na kushiriki mchezo huu.

Ndiyo maana hata leo nikaona nisimuache nyumbani, bora nije naye ajionee mwenyewe jambo jema alilonishauri na kutimia Mungu ambariki sana mke wangu Leyla”.

Alimaliza kusema mshindi huyo ambaye baada ya kukabidhiwa pikipiki yake alimpakiza mkewe na kuondoka nae huku akiwasisitiza wengine kuendelea kushiriki shindano hilo linaloelekea ukingoni ambapo mshindi anatarajiwa kuondoka na nyumba.
Washindi wengine watano waliojishindia ving’amuzi vya Ting HD kwenye droo hiyo wanatarajiwa kujulishwa hivi karibuni jinsi watakavyoweza kupatiwa zawadi zao.