×

Wakulima Kanda ya Kati Wahimizwa Kutumia Huduma za Kidijitali

DODOMA: Wakulima Kanda ya Kati wamehimizwa kutumia huduma za kifedha kidijitali zinazotolewa na Mixx by Yas ili kurahisisha upokeaji wa malipo ya mazao, kupata mikopo na kufanya miamala kwa usalama zaidi.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Biashara wa Mixx by Yas Kanda ya Kati, Charles Gasper, wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Gasper amesema kupitia huduma ya Mixx Kilimo, wakulima wanaweza kupokea malipo ya mazao moja kwa moja kupitia simu zao, kupata mikopo ya Kilimo Pesa inayofikia hadi Sh milioni 3, pamoja na kunufaika na huduma za bima ya afya ya mifugo.

Amesema matumizi ya huduma hizo yanawasaidia wakulima kupunguza utegemezi wa miamala ya fedha taslimu na kuwawezesha kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Kwa upande wake, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, amesema ushirikiano kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Ushirika na Mixx by Yas umechangia kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali miongoni mwa wakulima na vyama vya ushirika mkoani humo.

Chitinka amesema wakulima wengi sasa wameanza kupokea malipo ya mazao yao kupitia simu baada ya minada, hatua ambayo imesaidia kupunguza usumbufu wa kusafiri kufuata fedha pamoja na kuongeza usalama wa fedha za wakulima.

Aidha, amesema huduma za Mixx zimeendelea kuwezesha vyama vya ushirika na SACCOS mkoani Dodoma kufanya miamala kwa urahisi na kwa njia salama.

Ameipongeza Mixx by Yas kwa mchango wake katika kukuza matumizi ya huduma za kifedha kidijitali na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wakulima pamoja na wanachama wa vyama vya ushirika.

Maonesho ya Nanenane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi na kampuni mbalimbali kuonyesha huduma na teknolojia zinazolenga kuongeza tija, kuboresha maisha ya wakulima na kurahisisha shughuli za kilimo nchini.

Leave a Comment