×

A-Z Kidudumtu Cha Kwenye Mboga Kinachodaiwa Kuua Watu

Kidudumtu akiwa katika jani la mboga.

KUFUATIA kuwapo kwa hofu kubwa kwa watumiaji wa mbogamboga na matunda kuwa kuna kidudumtu ambacho ukikila kwenye mboga au tunda unaweza kufariki dunia, Amani limechimba na kuibuka na A-Z kuhusu mdudu huyo ambaye anakuwa gumzo kila kukicha.

Taarifa za kuwepo kwa kidudumtu zilianza kuenea kupitia mitandao ya kijamii huku picha ya mboga na matunda kama papai zikisambaa.

KUNA MTU ALIYEKUFA?

Katikati ya gumzo hilo, Amani lilizungumza na watu mbalimbali na kuweka mada hiyo kwenye mitandao  ya kijamii hasa makundi ya WhatsApp ambayo yamekuwa yakisambaza taarifa kwa haraka zaidi.

…akiwa kwenye Papai.

Kupitia makundi hayo, mwandishi wetu alitaka ajitokeze mtu au watu wenye ushahidi kama wamewahi kumuona mdudu huyo au ndugu kufariki dunia au kudhurika kwa kula mboga au matunda yenye kidudumtu. Lakini kupitia makundi hayo hakuna aliyetoa ushahidi wa kuthibitisha uwepo wa mdudu huyo zaidi ya kusikia tu.

MIKOANI KUKOJE? Baada ya kukosa mashuhuda waliomuona mdudu huyo, Amani lilizungumza na baadhi ya maofisa kilimo wa sehemu mbalimbali ikiwemo Dodoma, Mara, Mwanza, Kahama, Shinyanga na Tunduru ambapo baadhi yao walisema kuwa hawajapata kesi, vifo, madhara au uwepo wa kidudumtu isipokuwa kwa Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mayunga John ambaye alikiri kuonekana kwa mdudu huyo mkoani kwake.

 

KIDUDUMTU ALIIBUKIA WAPI?

Kwa mujibu wa Mayunga, kidudumtu huyo yupo na kwa mara ya kwanza alionekana Kandokando ya Ziwa Victoria eneo la Nkome ambako wananchi wa eneo hilo wengi ni wavuvi.

HUYU HAPA KIDUDUMTU

“Mdudu huyo ni kweli yupo na kwa mara ya kwanza alionekana kwenye mboga za majani kama kisamvu, mchicha na kwenye tunda la papai katika moja ya Masoko ya Nkome. KIDUDUMTU

ATUMIWA KIBIASHARA

“Baada ya kuonekana kwa mdudu huyo, inadaiwa kwamba, kuna baadhi ya wafanyabishara wa samaki na dagaa waliamua kumtumia mdudu huyo kama sehemu ya skendo kwa kuvumisha kuwa anaua ili watu waache kununua mboga za majani, ikiwemo kisamvu na mchicha ili wahamie kwenye samaki, maharage na dagaa.

WAFANYA BIASHARA WALIFANIKIWA?

“Ilidaiwa kuwa, kwa kiasi fulani wafanyabiashara hao walifanikiwa kwani hofu ya mdudu huyo ilizidi kuenea katika masoko mbalimbali ya Geita na watu wakapunguza kula mbogamboga na matunda.

AFARIKI KWA KULA KIDUDUMTU

“Kutokana na uvumi huo kuendelea kusambaa kwa kasi, watoto wa nyumba moja Kata ya Bugulula mkoani Geita waliugua ghafla. Wazazi wao waliwapa dawa za kienyeji, lakini kwa bahati mbaya mtoto mmoja alifariki dunia kutokana na zile dawa ndipo watu wakavumisha kuwa, mtoto huyo alifariki na mwenzake kuugua kwa sababu walikula mboga yenye kidudumtu.

UKIMGUSA KIDUDUMTU MWILI UNAVIMBA?

“Uvumi huo ukaendelea kuwa, ukimgusa mdudu huyo au ukigusa mboga au tunda lililotembelewa na kidudumtu basi mwili wako unavimba jambo ambalo halikuwa ukweli wowote.

SERIKALI KAZINI

“Kutokana na uvumi huo, kama serikali tuliingia kazini kwa kutembelea maeneo

mbalimbali ya  Nyankumbu, Mkolani, Mtakuja, Kasamwa na maeneo mengine ya vijijini kwa kuwatumia wataalam wetu wa kilimo kukusanya sampo mbalimbali za wadudu hao ili kuwalinganisha na wale wa awali ili kupata ukweli kama ni wa aina moja au la.

VIDUDUMTU WATUA MAABARA

“Tulipokusanya sampo mbalimbali za wadudu hao tuliwatumia wataalam wa Kilimo wa Ugiliguru jijini Mwanza na Taasisi ya Wadudu na Madawa Shinyanga kwa

ajili ya uchunguzi.

UKWELI KIDUDUMTU ANAUA?

“Kutokana na majibu ya wataalam, tuligundua mdudu huyo hana madhara na hakuna taarifa rasmi inayoonesha kuwa kuna mtu alifariki dunia kwa sababu ya kula mboga iliyokuwa na mdudu huyo.

KIDUDUMTU NI NINI? “Kidudumtu ni hatua ya tatu ya ukuaji wa kipepeo ambaye kabla hajawa kipepeo kamili, anapitia katika hatua zifuatazo;

HATUA YA KWANZA -YAI “Kipepeo huanza kwa kutaga

mayai ambayo huwa na gamba gumu liitwalo korioni (chorion). Mayai haya huwa yanatofautiana na aina ya spishezi za vipepeo, lakini yote huwa ya miduara.

HATUA YA PILI -FUNZA, LAVA AU KIWAVI

“Katika hatua hii, kipepeo hugeuka na kuwa kiwavi, lava au funza na anakuwa na uwezo wa kujitokeza sehemu ya kichwa na kuonekana kama nyoka. “Pia anakuwa na madoa kama macho na huwa na uwezo wa kutoa kemikali f’lani kwa ajili ya ulinzi wake.

HATUA YA TATU- BUNDO AU BUFA

“Hii ni hatua ya tatu ya kipepeo ambayo hujulikana kitaalam kama Bundo ambapo kipepeo anakuwa ameanza kukamilika na huanza kuzalisha homoni kadhaa. Kiwavi (hatua ya pili), huacha kula na kuanza kutafuta sehemu ya kutulia, hasa chini ya majani. Bundo kwa kawaida huwa hajongei, isipokuwa huweza kujitikisa, kujinyongany’onga na kutoa milio kadhaa kuwatishia maadui.

KWA NINI ANAFANANISHWA NA MTU

“Hutoa kipepeo anayefananishwa na mtu kwa sababu ya mabadiliko ya kawaida katika wadudu na siyo tu kufanana na mtu, bali anaweza kufanana na nyani, mbwa na vitu vingine. “Ukimuangalia vizuri ni kama ana mapembe, kidevu, tumbo na vingenevyo.

ETI MASHAVU NI MABAWA “Ukimuangalia kidudumtu

anaonekana kama ana mashavu ya binadamu, ule ni mkusanyiko wa mabawa na anakuwa na mabawa meupe yenye rangi nyeusi.

HATUA YA NNE- NDUMILI AU KIPEPEO

“Katika hatua hii ya mwisho, kipepeo anakuwa amekamilia, hatua ambayo watu wengi huiona pasipokufahamu jinsi anavyozaliwa hadi kufika hapo. “Kwenye hatua hii kipepeo huitwa ndumili. Huwa na mbawa ya mbele na nyuma na miguu sita. Kisha kutoka nje kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kuanza kujifunza kuruka.

KWA NINI ANAKAA KWENYE MATUNDA NA MBOGA?

“Mara nyingi vipepeo huwa wanapenda kuzaliana kwenye mimea yenye asili ya maziwa (milkweed) kama kisamvu, mpapai na mingineyo na ndiyo maana hata picha zinazosambaa zinaonesha akiwa kwenye papai na jani.

UKIMLA KIDUDUMTU KWA BAHATI MBAYA UNAKUFA?

“Hana madhara hata kama utamla kwa bahati mbaya kwenye mboga ila ni vyema kuwa makini kwa kusafisha mboga vizuri kwa sababu wakulima nao wanatumia dawa, hivyo usipoosha vizuri unaweza kula hata madawa ambayo hayakustahili.

KWA NINI WASIZALIANE PORINI?

“Miaka ya nyuma, Geita ilikuwa na mapori mengi sana na kulikuwa na aina nyingi za mimea ya maziwa, lakini kutokana na uharibifu wa mazingira, mimea hiyo imekuwa ikipungua siku hadi siku, mwisho wa siku, viumbe hao wanasogea kwenye mimea ambayo hutumiwa na binadamu.

ATHARI ZIKOJE KWA WANANCHI? “Hakuna vifo wala madhara mengine isipokua baadhi ya watu waliacha kula mbogamboga na matunda, wakulima kufyeka na kukata baadhi ya miti yao ya matunda na mboga kwa kuamini kidudumtu anaua.


MAKALA: GABRIEL NG’OSHA | AMANI

Leave a Comment