
LIGI za soka za Tanzania kwa sasa zimesimama, timu zinakaribia kuanza maandalizi ya msimu wa 2017/2018, wachezaji wengi wapo kwenye mapumziko pia, huku wengine wakiwa bado wapo kwenye michuano mbalimbali mifupi.
Wakati msimu wa 2016/17 ulipokuwa ukimalizika, kuna wachezaji ambao bila shaka walionyesha uwezo mkubwa na yawezekana wamekuwa na kawaida ya kuonyesha uwezo wa juu hata katika siku za nyuma, kiasi kwamba kwa soka wanalocheza wanao uwezo wa kucheza kwenye ushindani wa kimataifa nje ya Tanzania.
Katika medani ya Bongo Fleva kuna wimbo uliosabababisha kuwepo na msemo maarufu wa Bongo Bahati Mbaya, ambao unamaanisha kuwa kuna watu wamezaliwa Tanzania lakini kwa aina ya fani au uwezo walionao ni kama vile wamezaliwa bahati mbaya.

Inawezekana maana yake isiwe nzuri sana kiuzalendo lakini kwa kuwa ni msemo ambao haupotezi maana yoyote, hawa ni wachezaji ambao ni wazawa wa Tanzania lakini kwa vipaji walivyonavyo wanao uwezo wa kucheza nje na wakafanikiwa ila hawajafanya hivyo kutokana na sababu tofauti.
Aishi Manula
Kipa wa Azam FC ambaye anatarajiwa kusajiliwa na Simba baada ya kudaiwa kuwa kila kitu tayari na kilichobaki ni kusubiri muda wa mkataba wa Azam umalizike ili atangazwe kuwa mchezaji wa Wekundu wa Msimbazi.
Manula anao uwezo mkubwa, ana uzoefu pia wa kucheza mechi za kimataifa, kwa ufupi ndiye Tanzania One kwenye idara ya kusimama langoni. Yawezekana hajapata tu nafasi ya kucheza kimataifa lakini anazo sifa nyingi za kucheza kwenye ligi yoyote Afrika.
Simon Msuva
Winga wa Yanga ambaye kwa zaidi ya misimu miwili amekuwa mchezaji anayeonyesha uwezo wa juu, amekutana na changamoto nyingi za kimataifa na amepambana nazo.
Ana uwezo mkubwa wa kusaidia mashambulizi, kuongeza presha kwa wapinzani na kufanya mazoezi muda mwingi kumemfanya awe fiti. Kuna kocha mmoja alinidokeza wiki iliyopita kuwa kuna wakala mkubwa wa Ulaya ambaye amemtaja Msuva katika mazungumzo yao lakini wakala huyo hajawahi kumuona Msuva isipokuwa amesikia sifa zake tu.
Katika kiwango alichonacho sasa ni muda sahihi wa Msuva kuondoka Yanga na kwenda kucheza soka la kimataifa, kuendelea kuchelewa kunaweza kumpunguza morali au akapishana na muda sahihi ambao anatakiwa kwenda nje kucheza soka la kulipwa.

Himid Mao
Kiungo mkabaji wa Azam FC ambaye anasifika kwa kucheza soka la nguvu. Ni mzuri kwenye kukaba na ameonekana kuwa fiti kwa misimu kadhaa sasa, hivi karibuni alienda nje ya nchi kufanya majaribio lakini bado kuna ukimya. Akifanya hivyo mara mbili au tatu yawezekana akafanikiwa kupata timu ya kimataifa.

Ibrahim Ajibu
Kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye inaelezwa kuwa anaweza kutua Yanga, anajua soka, anao uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira, anajua kufunga lakini tatizo lake ni kuwa ‘anacheza soka’ na mashabiki. Aina ya uchezaji wake ni kama walivy-okuwa wakifanya wachezaji kadhaa mastaa wa zamani kama ilivyokuwa kwa Mrisho Ngassa, lakini kama Ajibu akiamua kutulia na kufanya kazi, bila shaka anaweza kufika alipo Mbwana Samatta.

Abdi Banda
Tangu akiwa anaichezea Coastal Union, alionyesha ni mchezaji mwenye kipaji, nahisi makuzi yanaweza kuwa yanachangia kutokuwa na nidhamu kwenye kazi yake ndiyo maana kuna wakati anaonekana ni mchezaji wa kawaida.
Anapokuwa uwanjani anajua anachokifanya, mzuri kukaba, mzuri kumtoa mpinzani mchezoni, ana bidii, tatizo lake ni moja tu nidhamu yake kutokuwa kwenye kiwango kizuri inasababisha baadhi ya watu wamuone ni mchezaji wa kawaida au ambaye hana mipango endelevu.

Mzamiru Yassin
Kiungo ambaye yawezekana hana nyota ya kutajwa au kuwa maarufu kama ilivyo kwa wenzake wa Simba lakini ni mwepesi wa kuelewa mafunzo na mara nyingi ameituliza timu ilipoonekana kuyumba. Anapocheza ni kama hayupo uwanjani lakini pasi zake na anavyozunguka kwenye nafasi vinamuongezea sifa ya kuwa aina ya mchezaji anayejitambua.
Mbaraka Yusuph
Mshambuliaji aliyekuwa akiichezea Kagera Sugar na sasa ametua Azam FC, licha ya umbo la wastani ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga na kuwa msumbufu kwa walinzi. Mbaraka anahitaji kuendelea kupata uzoefu zaidi wa mikiki ya kimataifa kwa kuwa bado hajazoea kukutana na walinzi wenye mbinu kali, akipita kwenye mitihani hiyo anaweza kuwa na uwezo wa kucheza nje ya nchi.

Ramadhani Singano
Alionyesha kwamba anaweza kuwa hatari alipokuwa akichipukia ndani ya Simba, mvurugano wa kimkataba na kisha baadaye kutua Azam FC vikamfanya ashuke kiwango na kuonekana ni mchezaji wa kawaida, kwa miezi kadhaa ameendelea kucheza katika kiwango cha wastani lakini kama akituliza akili kwenye kazi yake, naamini Singano bado anao uwezo mkubwa kuwa mchezaji tishio licha ya kuwa na umbo dogo.
Mohamed Ibrahim ‘Mo’
Kipaji chake kinaweza kuwa kinaendana na kile cha Ajibu, kilichomrudisha nyuma ni kuwa na majeraha ya mara kwa mara. Akitulia na kuwa fiti kisha akaamua kufanya kazi, Mo anaweza kuwa aina ya mchezaji ambaye klabu yoyote Afrika Mashariki itahitaji iwe naye, kinachoweza kumpunguzia maksi kwa sasa ni kuwa hana uzoefu wa mechi nyingi au mikiki mingi ya kimataifa.
Kenny Ally
Alionyesha uwezo mkubwa msimu uliopita kiasi cha kuwa chaguo la timu nyingi kumuwania wakati akiwa Mbeya City, lakini bahati ikawaangukia Singida United ambao wamemsajili.
Ni kiungo mzuri ambaye ana kipaji lakini kwa sasa kwenda nje bado ni mapema kwake kwa kuwa anahitaji kupata msimu mmoja wa kucheza kwa presha, akutane na upinzani mgumu na ikiwezekana aitwe katika timu ya taifa ndipo anaweza kuanza kufikiria kwenda nje kucheza soka la kulipwa.
Gadiel Michael
Beki chipukizi wa Azam FC ambaye amekuwa akionyesha aina ya uchezaji unaotakiwa kwenye soka la kisasa kwa beki wa kushoto kutumika kama winga wakati huohuo anakuwa na uwezo wa kukaba, ndivyo anavy-ofanya.
Kinacho-msaidia mbali na kuwa ana kipaji, pia anajituma na ni mwepesi wa kufanya maamuzi, umri wake nao ni mdogo na unaruhusu kumfanya ajifunze zaidi ili azoee mikiki, ushiriki wake katika michuano ya Cosafa unaweza kumsaidia kukua kifikra na kupata uzoefu. Akipata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao ngazi ya klabu, anaweza kukua zaidi na kuwa bora zaidi ya ilivyo sasa.
JOHN JOSEPH,