
Msanii wa muziki wa asili nchini Tanzania, Mrisho Mpoto maarufu kwa jina la ‘Mjomba’ amezidi kuwavuta Watanzania walio wengi kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kupitia Maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Mpoto ambaye ni Balozi wa Banda la Hifadhi ya Ngorongoro kwenye maonyesho hayo amekuwa akiamasisha utalii wa ndani kupitia nyimbo zake na mavazi yakwe pamoja na mbwembwe anazofanya akiwa kwenye Banda la Hifadhi hiyo ambapo wananchi wamekuwa wakimiminika kujioneavitu mbalimbali vinavyopatikana Ngorongoro.

Kamera ya Global Publishers imepenya mpaka katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Chang’ombe ambako maonyesho hayo yanafanyika na kujionea hamasa ikipamba moto hasa kupitia burudani zinazofanyika Banda hilo jambo ambalo limewavutia wengi.

Mrisho Mpoto ameeleza kuwa kupitia Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, wananchi wataweza kujionea wanyama na vitu vya asili ambavyo vinapatikana kwenye hifadhi hiyo wakiwemo tembo, simba, nyumbu, chui na wanayama wengine.

Mbali na hayo, Mpoto amewataka wananchi wananchi wafike katika banda hilo ili kuweza kujua vivutio mbalimbali vya hifadhi hiyo vinavyopatikana ambavyo ni asili ya Tanzania.




PICHA NA DENIS MTIMA | GLOBAL PUBLISHERS