
HIVI karibuni uongozi wa Simba ulikuwa na mpango wa kutaka kuachana na kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda, Jackson Mayanja. Inadaiwa kuwa sababu kubwa ya uongozi huo kutaka kuachana na Mayanja ni kwamba kocha huyo ameshindwa kuendana kiufundishaji na Omog ambaye ndiye bosi wa benchi la ufundi la timu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, uongozi huo uliona ni bora uachane na Mayanja ili uweze kumuajiri Mrundi, Niyongabo Amars ambaye tayari alikuwa katika mazungumzo mazuri na uongozi lakini juzi Jumatatu uongozi huo ulibadili mawazo na ukaamua kuachana na mpango huo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog alisema kuwa, alishangazwa na taarifa hizo za kutimuliwa kwa Mayanja klabuni hapo wakati msimu uliopita walifanya kazi vizuri tena kwa ushirikiano mkubwa. “Unajua baada ya kurejea nchini nilikutana na uongozi na tulijadili mambo mengi kuhusiana na timu.
“Lakini hakuna jambo lolote ambalo waliniambia kuwa wanataka kuachana na Mayanja, hata hivyo nilipopata taarifa hizo nilishituka sana, ikanibidi niwaulize viongozi na wakaniambia nisiwe na wasiwasi.

“Kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba Mayanja bado ni msaidizi wangu na jana (juzi) pamoja na leo (jana), tulikuwa pamoja mazoezini tukiendelea na majukumu yetu kama kawaida,” alisema Omog. Katika hatua nyingine, gazeti hili lilimtafuta Amars ili kujua mustakabali wake na Simba baada ya hivi karibuni kudai kuwa alikuwa katika mazungumzo na uongozi huo na muda wowote angetua nchini kwa ajili ya kumalizana nao.
“Bado sijatumiwa tiketi ya ndege kwani walisema watanitumia hivi karibuni ili nije Tanzania kwa ajili ya kumalizana nao. “Hata hivyo, sijui kama wamebadili mawazo kwa sababu bado hawajaniambia chochote na juzi tu (Jumapili) nilizungumza na kiongozi mmoja wa timu hiyo na akaniambia kuwa watanitumia tiketi hiyo lakini kama wamebadili mawazo mimi sina tatizo,” alisema Amars ambaye amewahi kuwa Kocha wa Timu ya Taifa ya Burundi, pamoja na Klabu za Telecom ya Djibouti na Bujumbura City ya Burundi.
Sweetbert Lukonge, Championi