
Mgombea urais kupitia wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya, National Super Alliance (NASA), Raila Odinga amepinga matokeo yanayoendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC. Odinga amesema kuwa, tume hiyo imekuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake bila kufuata utaratibu zinazofaa.
Waziri mkuu huyo wa zamani amesema kabla ya matokeo yoyote kutangazwa, IEBC inafaa kuwapa mawakala wa vyama Fomu 34A kutoka vituoni. Amesema kwa sasa, bila kuwepo kwa fomu hizo, ni vigumu kubaini matokeo yanayopeperushwa yanatoka wapi.
“Mfumo umeacha kufanya kazi. Sasa ni mitambo inayopiga kura. IEBC wamesema kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu 34A pekee zinazoonesha chanzo cha matokeo,” amesema.
“Kwa hivyo, tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka tume ya IEBC itoe Fomu 34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa.”
IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya urais mtandaoni, na kufikia saa 1:06 asubuhi, matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 7,163,684 (54.82%) na Raila Odinga wa ODM alikuwa na kura 5,794,443 (44.34%) ambapo matokeo hayo ni ya kutoka vituo 35095 kati ya 40883:
“Hii ni kompyuta inayopiga kura,” alisema Bw Odinga akikataa matokeo hayo.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanda katika kituo cha taifa cha kujumlishia na kutangaza matokeo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi. Matokeo yalianza kutiririka baadaye Jumanne jioni baada ya shughuli ya kuhesabiwa kura kuanza. Matokeo hayo yamekuwa yakionesha Bw Kenyatta akiongoza.
Wakala mkuu wa muungano huo wa upinzani, naibu waziri mkuu wa zamani Musalia Mudavadi alikuwa awali amehutubia wanahabari na kutaja matokeo yanayotangazwa na tume hiyo kama utapeli. Alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo kupuuzilia mbali matokeo yanayotangazwa.