
MAMBO yameanza kuwa mazuri kwani straika wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, jana Ijumaa aliwashangaza wengi katika mazoezi ya timu hiyo baada ya kufunga mabao saba.
Simba, jana ilikuwa ikifanya mazoezi hayo ya mwisho kwenye Uwanja wa Boko jijini Dar es Salaam kabla ya kuvaana na Azam, leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Mbagala.
Katika mazoezi hayo ambayo Championi iliyashuhudia, Mavugo alifunga mabao hayo kwa staili tofautitofauti na kumshangaza Kocha wa Simba, Joseph Omog.
Mavugo raia wa Rwanda amekuwa akipigiwa kelele za kukosa umakini anapokuwa uwanjani akikosa nafasi za wazi za kufunga anazozipata.
Akizungumza na Championi Jumamosi kuhusu uwezo huo wa Mavugo, Omog alisema: “Mavugo amenishangaza kwa leo (jana), ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga, akiendelea hivi atakuwa msaada kwetu.”
Wakati huohuo, Mshambuliaji wa Simba, Nicholaus Gyan, naye alifunga bao kali la ‘kideo’ katika mazoezi hayo na kumuacha kipa Aishi Manula asifanye lolote.
Gyan raia wa Ghana, alifunga bao hilo kwa staili ya ‘bicycle kick’ wakati akijiandaa na mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam.
Gyan alipata krosi safi na kufunga bao hilo ambalo liliwafanya mashabiki wa Simba waliokuwepo mazoezini hapo kulipuka kwa furaha na kumsifu straika huyo.
Akizungumzia kiwango cha Gyan, Omog alisema: “Ni mchezaji mzuri, anajituma sana akiwa mazoezini na hata kwenye mechi yupo hivi, kwa mwendo huu naamini tuna safu nzuri ya ushambuliaji msimu huu.”