×

Kocha Simba: Ajibu wa Sasa Anatisha

BAADA ya juzi Jumamosi, mshambuliaji Ibrahim Ajibu kuiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kocha mkuu wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, amesema kuwa Ajibu wa sasa ni moto tofauti na yule wa zamani.

Yanga imemsajili Ajibu hivi karibuni akitokea Simba kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji na tangu ametua kikosini hapo amekuwa na mchango

 mkubwa kwani mpaka sasa ameshaifungia timu hiyo mabao mawili kati ya manne ambayo imefunga mpaka sasa katika mechi nne za ligi kuu ilizocheza.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kibadeni alisema kuwa Ajibu kwa sasa anaonekana kukomaa kwani anajituma vilivyo uwanjani na anapambana, jambo ambalo hapo awali lilionekana kuwa ni tatizo kwake, licha ya kuwa na uwezo mkubwa.

Alisema hali hiyo ndiyo inayomfanya mpaka sasa kuwa mmoja kati ya washambuliaji wa Yanga waliofanya vizuri na kuiwezesha timu hiyo kujikusanyia pointi nane katika mechi zake nne ilizocheza.

“Nampongeza Ajibu kwa kubadilika kwani hivi sasa anaonekana kukomaa ukilinganisha na hapo nyuma wakati alipokuwa Simba.

“Hivi sasa anajituma vilivyo uwanjani, anapambana na ndiyo maana ameweza kufunga mabao mawili mpaka sasa kati ya manne ambayo Yanga imejikusanyia katika mechi zake jambo ambalo hapo nyuma wakati akiwa Simba lilikuwa ni tatizo kubwa kwake japokuwa alikuwa na uwezo mkubwa.

“Nimwombe tu kuwa, hapo alipofikia ajitahidi kwenda mbele zaidi asikubali kurudia tabia yake ya zamani kama kweli anataka kufika mbali kisoka kama ilivyo kwa Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji,” alisema Kibadeni.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam.

Leave a Comment