
MKURUGENZI wa Msama Promotions, wasimamizi na wasambazaji wa kazi za Muziki wa Injili, Alex Mwita Msama, amempongeza Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harisson Mwakyembe kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kupitia vyombo vya habari kuwa anaunga mkono kampuni inayopambana na wezi wa kazi za muziki za wasanii wanaouza CD feki.
Msama aliutaja Mkoa wa Mwanza kwamba angalau umepunguza uuzwaji na utengenezaji wa CD feki za kazi za wasanii na kuomba mikoa mingine inayoendelea na kadhia hiyo kuacha mara moja kwani oparesheni kali itawafikia siku yoyote.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Msama alisema kuwa siku na saa ya kuwakamata wezi wa kazi za wasanii haziko mbali kwani tayari wamekwishafahamika sehemu walipo na wanapozalishia CD hizo feki.
Alisema serikali inatengeneza mazingira safi na wafanyabiashara waaminifu wanaofuata utaratibu sahihi, ukiwemo ulipaji wa kodi kwa wakati na hivyo kampuni yake itaendelea kuhakikisha kazi za wasanii zinalindwa na kuheshimika ipasavyo.
Pia, katika kuonyesha msisitizo, Msama alisema: “Serikali ya awamu ya tano ni serikali ya kazi, hivyo haina chuki na mfanyabiashara yeyote anayefuata utaratibu wa kawaida ikiwemo kulipa kodi na mambo mengine ya kufanana na hayo.
“Nirudie tena wito wangu kwamba sasa biashara haramu ya kazi za wasanii basi, angalau kwa mkoa wa Mwanza matukio ya kurudufisha na kuuza CD feki yamepungua na hii yote ni kutokana na kampeni yetu ya kupambana na maharamia wa kazi za wasinii.
“Tutahakikisha tunawakamata wote watakaondelea na tabia hiyo kwani hata waziri Mwakyembe anakerwa na tabia hiyo ndiyo maana katika hotuba zake anajitahidi kukemea watu wa namna hiyo.
“Ninamshukuru Mkuu wa Polisi nchini, Simon Sirro, kwa kuwa tayari kutoa askari ambao tutashirikiana nao kuwakamata maharamia wa kazi za wasanii muda wowote.
“Tukiwaondoa wezi wa kazi za wasanii serikali itakusanya kodi halali. Kila mmoja awapige vita wachuuzi, wezi na maharamia wanaoiba kazi za sanaa kwa kuchoma CD feki, kwani kwa kufanya hivyo wananyonya jasho la wasanii na kuiingizia hasara serikali kwa kutolipa kodi halali.
“Sisi kama wasimamizi na wasambazaji wa kazi za sanaa tumeazimia kufanya ufuatiliaji kwa oparesheni maalum ambayo haina siku wala saa na hata atakayekutwa dukani kwake au nyumbani ameruhusu watu wakitengeneza au kuuza CD feki tutawakamata na wao kama maharamia.”
1. Mkurugenzi wa Msama Promotions ambao ni wasimamizi na wasambazaji wa kazi za Muziki wa Injili, Alex Mwita Msama, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
NA DENIS MTIMA/GPL