
WAKATI msimu wa Ligi Kuu ya Kikapu Marekani NBA ukianza mashabiki tayari wameshakaa sawa kushuhudia mechi kali ambazo zinatarajiwa kupigwa. NBA ndiyo ligi maarufu zaidi ya kikapu duniani ikiwa inawashirikisha mastaa wakubwa wengi kutoka sehemu zote kubwa duniani.
Wakati ligi hii ambayo imeanza rasmi jana, kuna wakongwe wanatarajiwa kuwika sana kwenye ligi hiyo na hawa ni baadhi yao: Vince Carter (Sacramento Kings): Unaweza kumuita ‘Air Canada’. Jina ambalo limekuwa likimtambulisha kwenye ulimwengu wa mchezo wa kikapu duniani.
Huu utakuwa msimu wa 20 wa staa huyo wa Kings kwenye NBA, na bado anatarajiwa kuwa anaweza kufanya mambo makubwa sana. Carter amewahi kutajwa kwenye kikosi cha All-Star mara tisa na amekuwa kwenye kikosi bora cha NBA mara mbili. Alifanikiwa kucheza michezo 73 msimu uliopita na kuwa na wastani wa pointi 8.0 rebaundi 3.1.

Bado anatarajiwa kuwika akiwa na umri wa miaka 40. Manu Ginobili (San Antonio Spurs): Ginobili hajawahi kushuka kiwango tangu alipoanza kutambulika kwenye NBA, msimu huu unaanza ukiwa ni wa 16 kwake lakini bado akionekana kuwa staa. Kwa kipindi cha miaka 15, alichocheza NBA amefanikiwa kutwaa ubingwa wa NBA mara nne, ametajwa kwenye kikosi bora cha NBA mara mbili. Msimu huu anacheza akiwa na miaka 40.
Thabo Sefolosha (Utah Jazz):
Unapowataja wachezaji wazaliwa wa Afrika kwenye NBA huwezi kuacha kumtaja staa huyu wa Utah Jazz pamoja na kwamba umri wake umekwenda. Huu utakuwa msimu wake wa 12 kwake kwenye NBA, amewahi kuwa beki bora wa msimu mara moja akiwa anatajwa kuwa huu utakuwa msimu wake muhimu wa kuonyesha kiwango chake cha juu akiwa na umri wa miaka 33.
Jamal Crawford (Minnesota Timberwolves):
Amekuwa akitajwa kama kiongozi kwenye kila kikosi ambacho amekuwa akikitumikia kutokana na jinsi ambavyo amekuwa akiwafundisha wachezaji chipukizi wa NBA. Msimu huu unakuwa wa 18 kwa staa huyo, kwenye NBA tayari akiwa na umri wa miaka 36, lakini anatajwa kuwa nguzo sahihi ya timu hiyo kwa msimu huu. Dirk Nowitzki (Dallas Mavericks): Dirk anatajwa kuwa atakuwa staa wa Milwa-ukee Bucks kwa msimu huu pamoja na umri wake kwenda kwa kasi.
Nowitzki anakwenda kwenye msimu wake wa 20 wa NBA, amefanikiwa kucheza michezo 1394 kwenye miaka 19, ameingia kwenye Kikosi Bora cha NBA mara 13, alikuwa MVP, mwaka 2007.
Pau Gasol (San Antonio Spurs):
Gasol ana umri wa miaka 37 kwa sasa na anakwenda kwenye msimu wake wa 17 kwenye NBA. Ana rekodi ya kutwaa ubingwa wa NBA akiwa na Los Angeles Lakers mwaka 2009 na 2010, anatajwa kuwa huu unaweza kuwa msimu wake wa mwisho kwenye timu hiyo, lakini bado anaaminika kuwa anaweza kuendelea kucheza NBA.