
KUELEKEA mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga dhidi ya Simba, presha imekuwa kubwa ambapo kila kona ya Jiji la Dar es Salaam gumzo ni mchezo huo wa wapinzani wa jadi.

Timu hizo zinakutana zote zikiwa zimetoka kuweka kambi nje ya jiji, ambapo Simba wao walikuwa Unguja wakati Yanga wao walikuwa Morogoro na inavyoonekana kazi itakuwa ngumu kwenye Uwanja wa Uhuru ambapo mchezo huo utachezwa, kesho Jumamosi.

Kituo cha runinga ya mtandaoni cha Global TV Online, leo Ijumaa kilirusha kipindi ambacho kilihusisha mashabiki wa pande hizo mbili chini ya udhamini wa Kampuni ya Sokabet na ‘povu’ lilimwagwa kwa wingi na mashabiki wa pande zote.

Mtangazaji wa Global TV Online, Easter Msofe ndiye aliyeongoza kipindi hicho kwa kuzungumza na mashabiki wa maeneo tofauti ikiwemo Ubungo na Magomeni jijini Dar.

Kila upande ulikuwa ukivutia kwake kuhusu mchezo huo wa leo, ambapo wale wa Yanga wengi wao walionekana kuwa na imani na mshambuliaji wao Ibrahim Ajibu na kiungo wao, Papy Tshishimbi na kudai kuwa wataongoza kuwamaliza Simba mapema.

Wale wa Simba wao walikuwa bize kujinadi kuwa Emmanuel Okwi atawalaza mapema Yanga kwa kuwa ni mzoefu na anawajua Yanga kwa kuwa amecheza nao mara nyingi.

Mbali na hapo, mashabiki hao walijipatia zawadi ya fedha kiasi tofauti kutokana na kujibu maswali kuhusu wanavyoifahamu Kampuni ya Sokabet ambayo inajihusisha na masuala ya kubashiri matokeo.

Baadhi ya mashabiki waliojipatia fedha ni Fumba Abdul Said na Nassor Meshack ambao walionyesha uhodari wa kufahamu jinsi Sokabet inavyofanya kazi ikiwemo na kutambua kuwa wao ndiyo wadhamini wakuu wa Majimaji, timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
