×

Niyonzima: Tunawajua, Hawatusumbui

Wachezaji wa Simba

KIUNGO mchezeshaji wa Simba Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ametamka kuwa wala hana hofu ya mechi ya leo dhidi ya Yanga, kwani wachezaji wao wengi wanawafahamu, hivyo hawatawasumbua.

 

Niyonzima aliyejiunga na Simba msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga, aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam kwa ndege kutoka kambini Zanzibar.

 

Yanga, leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo namba 58 wa Ligi Kuu Bara.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Niyonzima alisema mechi za Simba na Yanga huwa hazimpi tabu, kwani zinakutanisha wachezaji wenye uwezo sawa na kujuana.

 

Niyonzima alisema, kikubwa amewataka wachezaji wenzake kucheza bila ya presha ya mashabiki ambao ndiyo wanaofanya mechi kuongezeka ugumu na pale mchezaji anapopigiwa kelele anapokosea. “Siku zote hakuna mechi nyepesi, kikubwa kinachotakiwa ni kujiamini na kuachana na presha ya mashabiki ambao ndiyo wenye presha kubwa kuliko sisi wachezaji wenyewe.

 

“Ninaamini kama kila mchezaji akitimiza majukumu yake tutashinda, kwani tunawajua wachezaji wengi wa Yanga, hawa hawatatusumbua na niseme tu kuna mechi za kutusumbua lakini siyo hii ya kujuana.

 

“Kipa anatakiwa kudaka vizuri, beki naye azuie inavyotakiwa na viungo tucheze vizuri kwa kutibua mipango ya adui na kuanzisha mashambulizi yetu,” alisema Niyonzima.

Na Wilbert Molandi

Leave a Comment