×

Simba Sawa Lakini Ajibu Ni Wakuchungwa

Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu.

LIGI KUU Bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja kati ya mabingwa wa tetezi, Yanga dhidi ya Simba katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Licha ya hivyo, kesho Jumapili kutakuwa na mechi tano za ligi kuu kwenye viwanja tofauti baada ya kuisha kwa mchezo wa watani wa jadi. Katika mchezo huo, Yanga watakuwa wenyeji wa Simba ambao wanaongoza ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga, nyuma ya Yanga wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 15.

 

Hii ni mechi ya aina yake kwanza kabisa kwa sababu ya mechi ya mwisho waliyocheza kabla ya mchezo wa leo katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliomalizika kwa sare ya bila kufunga kabla ya kupigwa mikwaju ya penalti.

 

Matokeo hayo yanaonyesha mchezo jinsi utakavyokuwa mgumu kutokana na rekodi za timu zote mbili nje ya utani wao wa jadi, wote wameshacheza mechi saba, wote wameshinda mechi nne na kutoka sare mechi tatu ingawa wana tofauti na katika idadi ya mabao ya kufunga, Simba wamefunga mabao 19 na Yanga mabao kumi hiyo ndiyo tofauti yao.

Ukweli haitokuwa mechi rahisi kwa timu zote, kila mmoja atahitaji kutaka kuonyesha ubora wa timu yake hasa kutokana na matokeo ya mechi za mwisho, tumeshuhudia Simba wakishinda mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji kabla ya Yanga kuibuka na ushindi kama huo dhidi ya Stand United.

Ukiangalia matokeo hayo yameamsha morali ya mashabiki wa timu zote mbili lakini kwa upande wangu naona Simba wana nafasi kubwa ya kuweza kupata matokeo ya ushindi katika mchezo wa leo. Yapo mambo mengi ambayo yanachangia Simba kuweza kufanya vizuri dhidi ya Yanga kwa kuwa wapo katika molari kubwa pia kiu ya kutaka kuchukua ubingwa.

 

Macho ya wengi naamini yatakuwa kwa Emmnuel Okwi kutokana na kuwa kwenye kiwango bora tofauti na matarajio ya wengi na ikumbukwe aliitwa mhenga wakati anakuja lakini leo ndiyo kinara katika timu ya Simba na ligi kwa ujumla kwa kufunga mabao mengi.

 

Hivyo naamini hii itakuwa nafasi yake kubwa ya kutaka kuwaonyesha kuwa hajaisha maana amekuwa akifanya vizuri kazi yake wakati wote kwa kuhakikisha anafunga na kuisaidia timu yake lakini uzoefu wake wa mechi za watani utambeba kwa kiasi kubwa. Lakini kwa pande wa Yanga mshambuliaji wao, Ibrahim Ajibu amekuwa katika kiwango bora na amekuwa msaada kwenye timu yake kwa kuonyesha uwezo mkubwa katika kila mechi anayocheza na ndiye amekuwa staa kwa sasa kwenye timu hiyo.

 

Ajibu anaijua vizuri Simba licha ya kushindwa kufanya vyema katika mchezo wa Ngao ya Jamii lakini kwa ubora ambao yupo nao atataka kuwaonyesha Simba thamani yake ndani ya uwanja hivyo wanapaswa kumchunga. Kutokana na ubora wake Simba kuna haja kubwa ya kuweza kumuwekea ulinzi kama kweli wanahitaji matokeo katika mchezo huo kwa sababu amekuwa hatabiriki kwenye uchezaji wake na ukiangalia hata katika mechi zilizopita ndiyo utagundua mshambuliaji huyo ni wa aina gani.

 

Lakini katika hizi mechi pia kumekuwa na mambo mengi ambayo yamekuwa yakitokea baada ya mechi kumaliza na hili limekuwa likichagizwa na mashabiki, sitoshangaa kusikia wachezaji wa timu fulani kusemwa kuwa wamechukua fedha ikitokea wakafungwa au kocha kiwango chake kimeisha nadhani hiyo haitoweza kuwa sahihi katika kukuza mpira wetu.

 

Mwisho natarajia kuona mchezo utakaokuwa na mchezo wa kiungwana kwa sababu soka siyo vita haipendezi viongozi kugombana au kupeleka lawama kwa waamuzi, kitu cha msingi ni kuhakikisha kila timu inafikia malengo yake katika kupata pointi tatu ili kujitengezea mazingira ya kuchukua ubingwa mapema. Pia mchezo wenye nidhamu wa hali ya juu utakaotuonyesha pia tofauti kati ya Simba, Yanga na timu zingine shiriki ambazo nyingi ni mpya kwenye ligi. Ukiachana na mchezo huo ambao unavuta hisia za mashabiki wengi pia kesho Jumapili kutakuwa na michezo mingine ya ligi kuu, tunatarajia kuona ushindani mkubwa kwao kama ilivyokuwa kwenye michezo iliyopita.

Leave a Comment