

CHAMA cha makandarasi nchini (Contractors Association of Tanzania – CAT) kinatarajiwa kufanya mkutano wa kitaifa kwa mara ya kwanza katika historia ya ukandarasi ili kubadilishana uzoefu na kuangalia namna bora ya kuunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli katika kufanikisha ukuaji wa uchumi na viwanda nchini.
Akizungumzia na waandishi wa habari kuhusu siku ya mkutano huo ambayo ndiyo Siku ya Makandarasi Tanzania, Novemba 17, Mwenyekiti wa CAT, Mhandisi Lawrence Esili alisema wamechagua siku hiyo ili kutoa fursa kwa washiriki kati ya 200 hadi 300 kubadilishana uzoefu na kuangalia namna bora ya kuunga mkono harakati za serikali.
Mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Mhandisi, Joseph Nyamhanga, Katibu Mkuu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mkutano huu umeandaliwa kwa pamoja na vyama vyote vya wakandarasi vikiwemo Contractors Association of Tanzania (CATA), Tanzania Civil Engineering Contractors Association (TACECA) na Association of Citizen Contractors (ACCT).
“Washiriki watatumia fursa hii kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na hasa katika sekta ya maji, nishati, ujenzi wa miundombinu ya reli, bomba la Uganda na Tanzania la kusafirishia mafuta ghafi ya petroli, ujenzi wa makao makuu Dodoma, na kadhalika,” alisema Esili.
Wadau wa makandarasi waliofanikisha mkutano huu ni Commercial Bank Of Africa (CBA), National Microfinance Bank (NMB), Business Times Limited pamoja na wafadhili wengine.
NA DENIS MTIMA/GPL