
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameachiwa kwa dhamana leo Jumanne jioni baada ya kushikiliwa na polisi tangu alfajiri akihojiwa jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuhojiwa katika Kituo cha Polisi cha Chang’ombe mkoani Temeke, Zitto alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinani (DCI).
Zitto anatuhumiwa kwa makosa mawili ikiwemo kuchpisha taarifa kinyume na sheria ya makosa ya mtandao na kutoa takwimu za uongo jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya takwimu ambapo amehojiwa na kupewa dhamana huku akitakiwa kurudi kituoni hapo Jumanne ijayo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu amesema baada ya Zitto kuhojiwa kuhusu aliyozungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani zilizofanyika Kijichi Jumapili Oktoba 29,2017 aliachiwa kwa dhamana.
Shaibu amesema Zitto aliyewakilishwa na wanasheria Venance Msebo na Steven Mwakibolwa alidhaminiwa na watu wawili na alitakiwa kurudi kituoni hapo Jumatatu Novemba 6,2017. Hata hivyo, amesema alikamatwa tena.
Aidha Zitto amesema wanaisubiri serikali kwenda kujibu tuhuma hizo mahakamani. “Kama alivyoeleza mwanasheria, kama kuna makosa ambayo wao wameyaona, basitunawasubiri mahakamani tukafafanue. Tutakapokwenda mahakamani mtaona kitakachoendelea.
“Nilitarajia lazima ningekamatwa, nilikuwa nimejiandaa kwa hilo, kwa sababu Rais aliagiza nikamatwe, nisingekamatwa ningeshangaa,” alisema Zitto.