×

Watu Kichuyaa!! Aipaisha Simba Kileleni, Amfikia Ajibu

Kiungo wa Simba, jina kamili Shiza Kichuya.

GUMZO la kina Papy Kabamba Tshishimbi, Emmanuel Okwi na Ibrahim Ajibu ghafla limezimika, na sasa watu wanataja jina moja tu: Kichuyaaaa.

Kiungo huyo wa Simba, jina kamili Shiza Kichuya, jana alikuwa mtu muhimu kwa Simba alipoirudisha kileleni kufuatia bao lake safi alilofunga dakika ya nane akiunganisha pasi ya juu ya Jonas Mkude.

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa, jana Jumapili.


Sasa Kichuya amefikisha mabao mawili katika michezo miwili iliyopita, na tayari ana jumla ya mabao matano katika chati ya ufungaji, akiwa ameshamfikia staa Ibrahim Ajibu wa Yanga. Msimu uliopita, Kichuya
na mabao 12, wakati wafungaji bora Abdulrahiman Mussa wa Ruvu Shooting na Simon Msuva aliyekuwa Yanga walifunga mabao 14 kila mmoja. Hii inaonyesha kuwa Kichuya ameanza kasi yake ya msimu uliopita.

Umuhimu wa bao hilo ni kwamba limeipatia Simba pointi tatu muhimu ugenini na kuifanya kufikisha pointi 19, zinazoiondoa Azam kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mbeya City ilijitahidi kusawazisha bao hilo, hasa kupitia kwa kiungo wao, Eliud Ambokile ambaye alionekana kuisumbua vilivyo ngome ya Simba lakini hawakuweza kupata bao la kusawazisha.

Simba sasa wanakwenda katika mapumziko ya mechi za kimataifa, wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi, hatua ambayo itawapa hali ya kujiamini.

Simba wanaonekana kama wanasuasua lakini kwa muda mrefu wameongoza msimamo wa ligi hii ambayo msimu huu inaonekana kuwa ngumu kuliko ilivyozoeleka.

Lakini katika hali ya kushangaza, mashabiki wa Mbeya City walianza kurusha chupa za maji uwanjani kwa takriban dakika tano katika dakika ya 26, kutokana na kutokukubaliana na maamuzi ya mwamuzi.
Dakika ya 43, Erasto Nyoni alikosa bao lililoonekana la wazi, baada ya kupiga mpira uliombabua kipa wa City, Fikirini Bakari.

Dakika ya 47, Mrisho Ngassa alipewa kadi ya njano, baada ya kumchezea vibaya Emmanuel Okwi.
Dakika ya 57, Simba walimtoa Haruna Niyonzima na nafasi yake ikachukuliwa na Said Ndemla, na katika dakika ya 73, Mzamiru Yassin alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo.

Dakika za mwishoni, Kichuya alitoka na nafasi yake ikachukuliwa na Mohammed Ibrahim ‘Mo’.
Vikosi: Mbeya City; Fikirini Bakari, Elick Kyaluzi, Hassan Mwasapili, Ally Lundenga, Sankan Mkandawile, Babu Ally, Mrisho Ngassa, Mohammed Samata, Mohamed Mkopi, Omary Ramadhani na Eliud Ambokile.

Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, John Bocco, Emmanue Okwi na Shiza Kichuya.
Baada ya mchezo wa jana, Kichuya alipewa Sh 100,000 na mashabiki wa Simba kutoka Dar waliosafiri hadi Mbeya, pia akapewa viroba viwili vya mchele.

 

Leave a Comment