
KIUNGO wa Yanga, Thabani Kamusoko raia wa Zimbabwe, ameonyesha wazi kuumizwa na kukaa kwake nje ya uwanja kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu yanayomsumbua kwa muda mrefu sasa.
Kamusoko ambaye alisajiliwa na Yanga misimu miwili iliyopita akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, hivi karibuni anatarajia kuanza kuitumikia tena timu yake baada ya kukosekana katika mechi nne za Ligi Kuu Bara.
Kiungo huyo kabla ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, alifanikiwa kucheza mechi tano za mwanzoni msimu huu ambapo anatarajia kuonekana tena uwanjani kwenye mechi ijayo dhidi ya Mbeya City.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa juu ya majeraha hayo, Kamusoko amesema: “Hakuna kinachouma zaidi katika soka kama kuwa majeruhi kwa sababu unakosa vitu vingi sana vya kufanya kwenye kazi yako.
“Kwanza ni kushindwa kuitwa timu ya taifa, pia unakosa muda wa kuisaidia klabu yako, lakini nashukuru hivi sasa naendelea vizuri na muda si mrefu nitarudi uwanjani nikiwa fiti kabisa.”