
NOVEMBA 17, mwaka huu, Rais wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe alionekana hadharani kwa mara ya kwanza kutoka mikononi mwa jeshi la nchi hiyo.
Aliponea tundu la sindano kupinduliwa baada ya jeshi kudhibiti nchi hiyo kwa siku kadhaa, hali iliyosababisha hofu kubwa kwa wananchi wa taifa hilo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde alielezea kitendo hicho kama ‘mapinduzi ya kijeshi.’
Swali linaloulizwa kwa sasa ni hili, ni nini chanzo cha jaribio hilo lililoshindwa? Wapi Mugabe alikosea na hali hiyo inatoa picha gani kwa Zimbabwe na Afrika?

Kupata majibu ya maswali haya ni vizuri kuangalia japo kwa ufupi alikoitoa nchi hiyo na namna alivyonusurika kuondolewa madarakani.
Rais Mugabe ana mchango mkubwa kwa nchi hiyo na hatutakosea kama tukisema ni mzalendo wa kweli kwani ameipigania hadi tone la mwisho.
Ndiyo maana amesikika kwa nyakati tofauti akisema hatakubali nchi yake ibaki mikononi mwa mbwa huku akiwafananisha wengine na nyoka.
Aliingia madarakani mwaka 1980 na ametumikia nchi hiyo kwa miaka 37 na kurejesha ardhi iliyokuwa chini ya wageni mikononi mwa Wazimbabwe.
Huu ulikuwa ukombozi na hapa ndipo uadui mkubwa ulipoanza kati ya Wazungu na Mugabe na ndiyo chanzo pia cha kuwekewa vikwazo kwenda Ulaya na Marekani.
Yafuatayo ni mambo nane usiyoyajua kuhusu Rais Mugabe;
NI SHABIKI WA CHELSEA NA BARCELONA
Alipokuwa kijana, Mugabe alikuwa mzuri katika mchezo wa tenisi, kulingana na aliyekuwa mwalimu katika shule ya Wakatoliki alikosomea Mugabe.
Hata hivyo, aliposhindwa katika mchezo huo, aliuchukia moja kwa moja. Mugabe amekiri kuwa hakuwa mzuri katika mchezo wa kandanda alipokuwa mdogo, ila kwa sasa, anapenda kuutazama.
Kwa mujibu wa Rais Mugabe yeye ni shabiki wa Klabu za Chelsea na Barcelona barani Ulaya.

‘KUFUFUKA’
Kuhusu afya yake, alipohojiwa wakati mmoja alisema: “Nimekufa mara nyingi-hapo ndipo nimemshinda Yesu Kristo. Yesu alikufa mara moja na akafufuka mara moja,” alisema alipotimiza miaka 88.
Ingawa alilelewa katika familia ya Kikatoliki, alipohojiwa na Kituo cha Habari cha Afrika Kusini, SABC, miaka michache iliyopita, alisema yeye si Mkristo anayetumikia dini kwa sana.
SHABIKI WA KRIKETI
Kwa muda mrefu amedhihirisha hadharani mapenzi ya mchezo wa kriketi. Ni mlezi wa Jumuiya ya Mchezo wa Kriketi ya Zimbabwe na nyumba yake ipo karibu na uga wa michezo wa Harare.
“Kriketi inafanya watu wawe waungwana na pia inawafanya watu kuwa wema,” alikaririwa akisema hivyo miaka michache baada ya Zimbabwe kupata uhuru.
“Nataka kila mtu acheze kriketi Zimbabwe. Nataka nchi ya Zimbabwe iwe nchi ya waungwana.”
MAZOEZI NA VYAKULA
Mugabe anapenda kufanya mazoezi. “Mimi hujihisi mgonjwa wakati sijafanya mazoezi ya viungo vya mwili,” Mugabe alisema miaka sita iliyopita.
Huamka kati ya saa kumi na kumi na moja alfajiri. Siri nyingine ya maisha yake marefu ni kwamba anapenda sana ‘sadza’.
Hiki ni chakula cha kienyeji kinacholiwa sana Zimbabwe na ambacho kina virutubisho vingi muhimu. Havuti sigara lakini hunywa pombe kidogo.
ANA WATOTO WATATU
Ana watoto watatu na mke wake wa pili, Grace Marufu, aliyekuwa karani wake. Mtoto wao wa tatu alizaliwa 1997, mwaka mmoja baada ya wao kufunga ndoa.
Mwanaye wa kwanza, Nhamodzenyika, alifariki dunia kutokana na malaria akiwa na umri wa miaka mitatu Mugabe alipokuwa mfungwa wa kisiasa enzi za serikali ya Rhodesia.
ANAPENDA MUZIKI
Mwanasiasa wa Zimbabwe ambaye kwa sasa ni hayati, Edgar Tekere, alimwambia mwandishi wa BBC, Brian
Hungwe, kuwa alipokuwa akifanya maandalizi ya sherehe ya uhuru wa Zimbabwe, Mugabe hakumtaka mwimbaji Bob Marley aalikwe kutumbuiza watu ila alimtaka muimbaji maarufu wa Uingereza, Cliff Richard. Pia anampenda Mwimbaji, Jim Reeves.
UVAAJI NGUO
Anapenda sana suti zinazoutosha mwili wake sawasawa na tai zinazofanana na kitambaa. Huwavutia sana wanamitindo nchini Zimbabwe kwa mavazi yake.
ELIMU YAKE
Kwa jumla, Mugabe ana shahada saba. Digrii yake ya kwanza ni kutoka Chuo Kikuu cha Fort Hare, Afrika Kusini.
Alisomea shahada zake nyingine kupitia mtandao akiwa gerezani. Shahada hizo ni za elimu, sayansi, sheria na usimamizi.
Kifupi; huyo ndiye Rais Robert Gabriel Mugabe, mkongwe wa siasa barani Afrika.
MAKALA: Julian Msacky