

JUKWAA Huru la Wazalendo Tanzania (Juhwata) limempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kwa kusimamia maslahi ya taifa ndani ya Bunge kwa kuunda kamati mbalimbali ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kutimiza azma ya Rais Magufuli ya kuhakikisha Tanzania inanufaika na raslimali za nchi yetu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Masiga Gulatone, amemwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na weledi wake uliotukuka kuunda tume ya wataalam kuchunguza sekta ya maliasili kama vile, wanyamapori, misitu na utalii.
“Rais bila woga amekuwa akitimiza wajibu wake kwa taifa letu hivyo tuendelee kumwombea na kumuunga mkono katika vita hii ya uchumi badala ya kukubali kugawanywa na vibaraka wa mabepari ambao wanatimiza majukumu yao dhidi ya taifa letu,” amesema Gulatone
“Jukwaa linaungana na Watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi yetu kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Dkt. John Pombe Magufuli ya kutuongoza na kututumikia watanzania wote kwa moyo wa kizalendo na ujasiri mkubwa” alisema Gulatone.