
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Fatema Dewji, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa shindano la Zawadi ya Chini ya Kizibo (UTC) la ‘Pindua Ushinde’.



KAMPUNI ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) leo Februari Mosi imezindua shindano la Zawadi ya Chini ya Kizibo (UTC) lijulikanalo kama “Pindua Ushinde” litakalofanyika kwa muda wa siku 45, linalotarajiwa kuisha Machi 10 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa shindano hilo, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni hiyo, Fatema Dewji, ameeleza namna ya kushiriki shidano hilo kwamba ili ujishindie zawadi, kinachotakiwa ni kununua maji ya Mo Maisha au Masafi yenye ujazo kuanzia mililita 600 hadi lita 1.7.
“Niwaambie Watanzania kwamba ni historia kwa nchi yetu kuwaletea shindano la zawadi ya Chini ya Kizibo kwa bidhaa za maji ya Mo Maisha au Masafi yenye ujazo kuanzia mililita 600, na mengine yanayozalishwa na kampuni yetu yaliyo katika vifungashio vya chupa za plastiki, ambapo hii haijawahi kutokea popote kutoka makampuni mengine,” amesema Fatema.
Amesema ‘Pindua Ushinde’ inakupa fursa ya kujishindia zawadi ya maji ya bure au pesa taslimu kuanzia Sh. 1,000 hadi 100,000, ambapo ili kujionea ulichoshinda, unatakiwa kupindua kizibo cha chupa ya maji ya Mo Maisha au Masafi.
Amefafanua kuwa maji yanayozalishwa na kampuni yao ni safi na salama kwa afya ya mtumiaji na hutayarishwa katika mazingira yenye ubora wa hali ya juu kutokana na kukidhi viwango vya kimataifa.
“Tutatoa ushirikiano kuondoa chupa za plastiki zitakazoonekana mitaani ili zitumike kama malighafi katika uzalishaji viwandani. Hii si mara ya kwanza kufanya kampeni za utunzaji mazingira, awali MeTL ilifanya kampeni ya utunzaji mazingira kwa kusafisha ufukwe wa Coco Beach,” aliongeza.
Kwa uapnde wake Meneja Mauzo wa Kiwanda cha A 1 kilicho chini ya Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited, Godfrey Mangungulu, amesema washindi wa maji ya bure na fedha kuanzia 1,000 hadi 50,000 watapewa zawadi zao waliponunua maji hayo na watakaoshinda zaidi ya fedha hizo watachukua bidhaa zao kwenye Kiwanda cha A1 kilichopo Kurasini.
“Tumeamua kurudisha fadhila kwa jamii kwani kwa zaidi ya miaka 20 tunauza bidhaa zetu, hivyo tumeamua kurudisha sehemu ya mauzo ya bidhaa zetu kwa jamii. MeTL tunajivunia bidhaa bora na usambazaji wetu unafika nchi nzima,” amesisitiza.