
BAADA ya kulazimishwa sare dhidi ya Mtibwa Sugar mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Sokoine, kikosi cha Mbeya City, jana Alhamisi asubuhi kilisafiri kuelekea mkoani Ruvuma.
Mbeya City ambayo imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 13, itashuka kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea kupambana na Majimaji wikiendi hii.

Msemaji wa kikosi hicho, Shah Mjanja ameliambia Championi Ijumaa kuwa, timu hiyo imesafiri huku wachezaji wakiwa na morali ya juu kuelekea mchezo huo.
“Timu imesafiri kuelekea mkoani Ruvuma ambako itacheza mchezo dhidi ya Majimaji kisha itasafiri kuelekea mkoani Mtwara ambako itacheza na Ndanda FC kabla ya kurejea mkoani Njombe kucheza na Njombe Mji kwenye Uwanja wa Sabasaba,” alisema Mjanja.
Wakati Mbeya City wakienda Songea, wapinzani wao wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons, wao watakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine kesho Jumamosi wakiwakaribisha Njombe Mji katika muendelezo wa ligi kuu mzunguko wa pili.
Prisons ni miongoni mwa timu zilizosonga mbele kwenye michuano ya Kombe la FA baada ya katikati ya wiki hii kuiondoa Burkina Faso kwenye michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti.
Katika michezo miwili ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, Prisons waliambulia vipigo kutoka kwa Azam FC na Singida United na kujikuta wakibaki na pointi zao 21 tu.