
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre, juzi alimuulizia kiungo mkabaji wa Yanga Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
Mfaransa huyo, alimuulizia kiungo huyo mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kwa Yanga kutoka sare ya bao 1-1 na Singida United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Kocha huyo, juzi alikuwepo uwanjani hapo akifuatilia mchezo huo huku akiwa na kitabu na kalamu akiwa anaandika baadhi ya vitu katika kitabu chake.

Akizungumza na Championi Ijumaa, mara baada ya mechi hiyo, alisema katika mechi hiyo hajamuona kiungo anayevaa jezi namba 13 (Kamusoko), sijajua tatizo nini, ninaamini kutokuwepo kwake na baadhi ya wachezaji nyota huenda ikawa tatizo kwao Yanga kupata matokeo hayo.
“Siyo vibaya kuja uwanjani kuwaona wapinzani wako, lengo ni kuwaona Yanga na Singida ambao hivi karibuni nitakutana nao.
“Kama yalivyokuwa malengo yangu ni kushinda kila mchezo ili tujiwekee mazingira mazuri ya ubingwa wa ligi kuu msimu na ili nipate matokeo mazuri.
“Sijamuona kiungo wa Yanga anayevalia jezi namba 13 (Kamusoko) sijajua tatizo ni nini, lakini nimebahatika kuwaona hao baadhi ambao nitakwenda kuwafanyia kazi,” alisema Lechantre.