
WAKATI homa ya mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga ukianza kupamba moto, kiungo wa Simba, Jonas Mkude amedai kuwa kama Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina ameachana na klabu hiyo, kipigo cha mabao 5-0 ambao walikitoa msimu wa 2011/12 kinaihusu tena timu hiyo.
Simba na Yanga zitapambana tena msimu huu Aprili 29, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa ligi kuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkude alisema kitendo cha Lwandamina kuachana na klabu hiyo wakati ikiwa bado haijacheza na Simba ni pigo kubwa kwa timu hiyo kwani anaamini hali hiyo itawavuruga kisaikolojia baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, hasa wale waliokuwa na mahusiano naye mazuri.

“Lwandamina alikuwa ni bonge la kocha ambaye kila mtu aliona mchango wake kwa Yanga, kama ameondoka kweli hilo ni pigo kubwa kwao.
“Lakini pia ni jambo zuri kwetu kwa sababu linaweza kutusaidia tukarudia kuandika rekodi yetu ya msimu wa 2011/12 ambapo tuliifunga Yanga mabao 5-0 tulipokuwa na kikosi bora kama kilivyo hiki cha sasa ambapo kulikuwa wakali kama Emmanuel Okwi, marehemu Patrick Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’, Kelvin Yondani na wengine wengi,” alisema Mkude.
Stori: Sweetbert Lukonge