
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwashughulikia viongozi wa serikali wanaowahamisha watumishi wa Umma bila kuwalipa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
Magufuli amesema hayo leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa Rais Magufuli ambapo amesema jambo la kuhamisha wafanyakazi bila kuwalipa ameshapiga marufuku hivyo kama kuna viongozi ambao bado wanakiuka agizo hilo hivyo ni lazima washugulikiwe.
”Iwapo atakuwepo na Mkurugenzi auma kiongozi yeyote wa Serikali yangu anamuhamisha mfanyakazi, awe mwalimu au mtumishi yoyote bila kumlipa posho yake ya uhamisho na bado huyo kiongozi anaendelea kufanya kazi, Waziri Mkuu lisimamie hilo,” amesema Magufuli.
Aidha, Risala ya Chama Cha Wafanyakazi nchini TUCTAikisomwa mbele ya Rais Magufuli ilieleza kwamba, licha ya kuwepo kwa zuio la Rais, lakini bado wafanyakazi wanahamishwa bila kulipwa stahiki zao jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kazi hapa nchini.
Hata hivyo, Rais Magufuli amesema iwapo kiongozi atamuhamisha mfanyakazi, lazima alipwe stahiki zake kwanza vinginevyo huyo kiongozi ni jeuri na dawa yake ni kumuondoa hivyo Mawaziri wanaohusika walifanyie kazi.