Ziara ya Rais John Magufuli, inaendelea mkoani Morogoro ambapo leo Mei 7, ametembelea Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kukipongeza chuo hicho kwa tafiti mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, uvuvi, panya kubaini mitego ya mabomu na ugonjwa wa kifua kikuu huku akisema wanao uwezo wa kuwafanya panya hao wakagundua pia waathirika wa UKIMWI.
Rais Magufuli ameambatana na mkewe, Mama Janeth Magufuli na viongozi mbalimbali wakiwemo, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt Steven Kebwe na wengine.
Akihutubia Chuoni hapo, Rais Magufuli amesema;
“Hakuna Chuo Kikuu chochote nchini cha kuendeleza Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, ni SUA pekee, ndiyo maana nimekuja kuwapa hamasa, mchape kazi, tembeeni kifua mbele. Leo nilitakiwa niwe nimeondoka Morogoro, lakini nikasema siwezi kuondoka mpaka nikutane na ndugu zangu wanaosoma na wanaofanya kazi Chuo Kikuu pekee Tanzania (SUA).
“Tafiti za kipekee zilizofanywa na chuo hiki, mojawapo ni ile ya kumfundisha panya namna ya kutegua mabomu pamoja na kubaini wagonjwa wenye kifua kikuu. Mnaweza kuwafanya hawa panya wakanusa hata mwenye UKIMWI akabainika, lakini nafahamu hamtaki kwa sababu huyo panya anaweza kukunusa hata wewe halafu ikawa tatizo.
Akizungumzia kuhusu utalii, Rais amesema;
“Iwapo nchi haina ndege haiwezi kupata watalii kwa sababu hawaji kwa mikokoteni wala kwa bodaboda ama baiskeli, ndiyo maana wenzenu tumeamua kununua ndege saba, mbili ni kubwa zinaweza kubeba abiria 264, zinaweza kutoka hapa mpaka Marekani bila kusimama.
“Wafugaji wetu wamekuwa wa kuzunguka kisa hawana soko la kueleweka la mifugo yako, hii imetengeneza mapigano sababu hakuna pa kupeleka mifugo yao. Huwa najiuliza, hivi sisi tuna kasoro gani, tuna ugonjwa gani? Tulipokosea ni wapi? Hakuna cha kutafuta mchawi kwa sababu sisi sote tulikuwepo wakati haya yanatokea.
“Mimi ninaamini Chuo Kikuu hiki cha SUA kinaweza kikawa chanzo kikubwa cha kubadilisha maisha ya Watanzania wengi.”