
SIMBA wameendelea kufanya kufuru nyingine ya fedha kwa kumsaini mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Meddie Kagere raia wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, kwa dau la dola 50,000 (sawa na shilingi 113,087,000).
Mshambuliaji huyo alitua nchini juzi Jumatatu alfajiri kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Simba, kabla ya kumsajili kwa dau hilo akiwa ameongozana na meneja wake, Gakumba Patrick.
Kagere ni usajili wa nne kwa upande wa straika ndani ya Simba katika kipindi hiki baada ya awali kusajiliwa kwa Adam Salamba, Marcel Boniventure na Mohamed Rashid.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, mshambuliaji huyo mara baada ya kutua, haraka mabosi wa Simba walimkimbiza katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach jijini Dar kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo.

Mtoa taarifa huyo alisema, mshambuliaji huyo aliyekuwa Mfungaji Bora wa SportPesa Super Cup, mwaka huu, alisaini mkataba wa miaka miwili juzi Jumatatu jioni kwa dau hilo.
Aliongeza kuwa, tofauti na dau hilo la usajili, pia mshambuliaji huyo atakuwa analipwa dola 5,500 (sawa na shilingi 12,439,500) kwa mwezi kwa kipindi ambacho atakuwa akiichezea Simba.
“Kagere tayari amesaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la dola 50,000, hiyo ni baada ya kufikia makubaliano mazuri kwa pande zote mbili.
“Alifika nchini Jumapili alfajiri akiwa na meneja wake na mkataba huo alisaini jana jioni (juzi), hivyo atakuwa sehemu ya wachezaji watakaocheza michuano ya Kagame,” alisema mtoa taarifa huyo.
Baada ya Kagere kuondoka Gor Mahia, klabu hiyo imetangaza kumsajili mshambuliaji raia wa Uganda, Erisa Ssekisambu, akitokea Vipers ya nchini humo ili kuziba pengo hilo.
Simba hivi sasa inajiandaa na michuano ya Kagame itakayoanza keshokutwa Ijumaa na inafanya usajili wa maana ili tu iweze kushiriki vema kwenye michuano hiyo na mingine inayowakabili msimu ujao.
Simba licha ya kupania kufanya vema kwenye michuano ya Kagame, lakini pia inataka kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, pamoja na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao ambapo itaanza Novemba, mwaka huu.