×

Ajali ya Lori, Hiace 3, Mbeya Dakika 20, Vifo 20

HUU ni msiba msiba mzito! Ndivyo uavyoweza kusema kufuatia ajali iliyoababisha vifo vya watu 20 ambavyo vimetokea ndani ya dakika ishirini.

Ajali hiyo iliyohusisha lori na daladala tatu, ilitokea juzi katika mteremko wa Iwambi eneo la darajani Mbalizi mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea majira ya mchana ambapo ilisemekana lori hilo lilifeli breki na kwenda kugonga daladala hizo tatu kwa mpigo zilizokuwa zinatokea stendi ya Mbalizi kuelekea Mbeya Mjini.

Kwa takriban dakika ishirini tangu ajali hiyo itokee, watu waliowahi eneo la tukio waliweza kubaini vifo hivyo 20 na kuanza kutafuta msaada wa namna ya kuwaokoa wale waliokuwa wamelaliwa na lori.

Taarifa za awali zilieleza kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni ‘kufeli’ kwa breki za lori ambalo lilikuwa linashuka kutoka mlimani.

“Inaonekana lile lori lilifeli breki sasa wakati dereva anahangaika nalo kuhakikisha anashuka nalo likiwa barabarani ndipo alipogonga daladala hizo kwa mpigo,” alisema shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwakipesile.

Naye shuhuda mwingine wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la John Chali, alisema kutokana na lori hilo kuwa na mzigo, baada ya kugonga daladala hizo, kwa pamoja zilitupwa katika bonde lililopo eneo hilo kisha nalo likafuata ambapo liliangukia moja ya daladala hizo.

“Yani daladala zilibingilika hadi kule bondeni na lile lori likaja kulalia moja kati ya zile daladala hivyo kusababisha baadhi ya watu kulaliwa na lori ndani ya daladala,” alisema.

UOKOAJI WAFANYIKA

Uwazi lilikuwepo eneo hilo na kushuhudia shughuli mbalimbali za uokoaji zikifanyika kwa tabu kutokana na lori hilo kulalia daladala.

WATU WAFURIKA

Wakati zoezi la uokoaji wa watu waliokuwa wamenasa kwenye ajali hiyo likiendelea, umati mkubwa wa watu ulikuwa umezunguka eneo hilo ili kutambua baadhi ya ndugu zao.

MAKALLA AONGOZA UOKOAJI

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alikuwapo eneo la tukio ambako kazi ya uokoaji ilishirikisha wananchi wa kawaida na vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Baadhi ya miili iliyokuwa ikitolewa katika ajali hiyo ilionekana kuharibika vibaya hususan ile ya abiria ambao walikuwa kwenye daladala ambayo ilikuwa imelaliwa na lori.

“Inauma sana jamani, wengine walikuwa wanalalamika kubanwa kwa muda mrefu sasa hadi wanakuja kuokolewa tayari wanakuwa wameshakufa,” alisikika mkazi mmoja wa Mbeya aliyekuwa anazungumza kwa uchungu huku akiangua kilio.

WAOKAAJI WAZIMIA

Baadhi ya watu waliofika katika eneo la ajali kwa lengo la kuokoa, walijikuta wakizimia baada ya kuona miili ikiwa imeharibika vibaya.

USHIRIKINA WATAJWA

Baadhi ya mshuhuda waliokuwa na imani haba, waliihusisha ajali hiyo na mambo ya kishirikina kutokana na mazingira ya eneo la ajali.

“Hapa kuna kitu tu we angalia hata damu hakuna sana lakini watu wamekufa kwelikweli. Halafu kama hiyo haitoshi, hii si mara ya kwanza ajali zinatokea eneo hili,” alisikika shuhuda mmoja akisema na mwingine kudakia:

“Kweli kabisa, aina ya ajali yenyewe ni imekaa kiajabuajabu, inawezekana kuna kitu kinasababisha ajali hizi na ndiyo maana hata damu za marehemu zimezua utata, siyo nyingi ukilinganisha na majeruhi na hata waliofariki.”

MADEREREVA WATAHADHARISHWA

Wakazi mbalimbali wa eneo lililotokea ajali waliwatahadharisha madereva kuwa makini na eneo hilo kwani limekuwa likitokea ajali mara kwa mara.

“Hili eneo kwa kweli linahitaji umakini sababu kuna mteremko hivyo ni vyema madereva wakawa wanakagua breki zao kabla ya kuanza safari ili kuepusha ajali.

“Kama mnakumbuka hapahapa ndipo alipowahi kupata ajali Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Mary Mwanjelwa na mara kwa mara ajali nyingi ambao hazileti madhara makubwa zimekuwa zikitokea hapa,” alisema Christopher Mwaisapila, mkazi wa Nzovye Mbeya.

Mashuhuda mbalimbali wa ajali hiyo walisema ni msiba mzito kwani umeondoa uhai wa watu wengi kwa wakati mmoja huku baadhi ya majeruhi zaidi ya 45 wakiwa kwenye hali mbaya.

“Ni msiba mzito kwa wana Mbeya na taifa kwa ujumla, kwa kweli tunamuomba Mungu pia atuepushie hizi ajali maana zimekuwa ‘too much’,” alisema shuhuda mmoja aliyekuwa eneo la ajali.

KAMANDA ATHIBITISHA

Mara baada ya zoezi la uokoaji kukamilika, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mussa Taibu alithibitisha kuwa ajali hiyo imeua watu 20 huku majeruhi wakilazwa katika Hospitali ya Ifisi na wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

UPEPO SIO MZURI

Wimbi la ajali linaonekana kuongezeka katika maeneo mbalimbali nchini kwani Juni 25, mwaka huu, watu 14 walifariki katika ajali iliyohusisha lori na daladala katika eneo la Dunani mkoani Pwani.