
WIZARA ya Afya nchini imesema kufuatia kuwepo taarifa za mlipuko wa pili wa corona katika nchi jirani, imekuwa ikipokea maswali mengi, watu wakiuliza iwapo wizara hiyo ina mpango wa kupokea chanjo ya corona na njia zipi zitumike kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na virusi vya corona.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Februari 1, 2021 na Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dodoma.
“Kwa sasa wizara haina mpango wa kupokea chanjo ya corona inayoripotiwa kuwepo na kutumika kwenye mataifa mengine, serikali kupitia wizara inazo taratibu zake za kufuata inapotaka kupokea bidhaa za afya, baada ya kujiridhisha, kwa nia njema kabisa ni hadi tujiridhishe.
“Kuhusu mbinu za kujikinga na corona, wananchi wajielekeze kwenye elimu inayotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kuimarisha usafi wa mazingira na wa mtu mmojammoja, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, sanitizer, lishe, kujifukiza, mazoezi, matumizi ya Ttba asili, n.k.
“Wizara ya Afya kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali imehakiki bidhaa kadhaa za tiba asili na kubaini zimekidhi vigezo vya usalama kwa ajili ya matumizi, bidhaa hizi tayari zinatumika na wengi zimewasaidia ikiwemo mimi waziri wa afya na familia yangu.
“Nalielekeza Baraza la Tiba Asili, kwa ushirikiano na watengenezaji wa bidhaa za tiba asili ambazo zimehakikiwa na Mkemia wa Serikali, kesho lifafanue zaidi juu ya bidhaa hizo kuwa zinafaa kwa matumizi na zinawaponya wengi au kuwapa nafuu, lengo watu wajue zinakopatikana.
“Naelekeza wataalamu wote Tanzania wa tiba asili watoe elimu ili kuelimisha Jamii, na wataalamu ambao hawajajitokeza wajitokeze ili dawa zao zihakikiwe na Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuhakikiwa na baraza letu la Tiba Asili”
“Baadhi ya bidhaa za tiba asili zilizohakikiwa na Mkemia Mkuu kuwa ni salama ni pamoja na Covidol, Bingwa, Nimcaf, Planet, Uzima, Bupiji, n.k; hizi ni baadhi tu. Kesho Baraza la Tiba Asili litataja nyingine, hizi ni silaha zetu tumepewa na Mungu kama nchi nyingine walivyopewa
“Nazikumbusha taasisi zote za umma, taasisi za kidini, taasisi binafsi, taasisi za kijamii na vyombo vyote vya habari kuepuka kutoa taarifa za afya ambazo hazifuati miongozo ya wizara, kwani wakishatoa taarifa hizo zinazua taharuki na hofu kwa jamii,” amesema Gwajima.