×

Lebron Apagawisha Mashabiki Wa Lakers

LeBron James.

MASHABIKI wa timu ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Lakers juzi walipagawa kwa shangwe wakati wakimpokea staa mpya wa timu hiyo, LeBron James.

 

LeBron aliibuka kwenye Uwanja wa Thomas & Mack jijini Las Vegas, ambako timu ya yosso ya Lakers ilikuwa inacheza dhidi ya wenzao wa Detroit Pistons kwenye michuano ya vijana ya majira ya joto ya Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA).

 

Staa huyo aliibuka akiwa amevalia kaptura akiwa amefuatana na mwenzake Brandon Ingram, ambapo mashabiki wa Lakers walianza kushangilia na kusimama na kuanza kumpigia makofi.

 

LeBron na Ingram walikwenda kuangalia mechi ya robo fainali baina ya Lakers na Pistons, ambapo timu hizo zilikuwa zinawania kucheza kwenye nusu fainali.

 

Mashindano ya majira ya joto ya mpira wa kikapu yanashirikisha timu za yosso za NBA na yanaendelea sehemu mbalimbali za Marekani.

 

James hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka minne wa kuchezea Lakers ukiwa na thamani ya Dola milioni 153.