×

Sanga Kajiwahi Tu, Ilikuwa Lazima Aondoke Yanga

Clement Sanga

JUZI Jumatatu moja ya mambo ambayo nilikuwa nikiyafikiria ili­kuwa ni juu ya mwelekeo wa Yanga lakini hasa ni kuhusu aliyekuwa Kai­mu Mwenyekiti wa kla­bu hiyo, Clement Sanga.

 

Nilijuliza inakuwaje Sanga anaendelea kuwa kion­gozi wa klabu hiyo waka­ti inaelekea shimoni na hakukuwa na dalili nzuri za kuinusuru inapoelekea klabu na timu kwa jumla.

 

Sanga ni mmoja wa vi­ongozi wazoefu kwenye soka la Tanzania, anazo sifa za kuwa kiongozi mzu­ri japokuwa kuna wakati huwa nawaza yawezekana kukaa kwake chini ya ki­vuli cha Yusuf Manji ndiko kuliko mfanya aonekane kiongozi mzuri, Labda!

 

Tangu kuondoka kwa Manji, Yanga ilionekana kukosa mwelekeo mzuri, timu na klabu kwa jumla vyote vilianza kupoteza dira na ikaonekana kama nguvu ya kumtegemea mtu mmoja ndiyo iliy­okuwa ikiwatafuna Yanga.

Juhudi za hapa na pale zikawa zinafanyika, lakini kuondoka kwa Manji ku­kafumbua mambo mengi na kuonyesha walijisa­hau na kuamini Manji ni Yanga na Yanga ni Manji, hivyo hawakuwa tayari ki­saikolojia kujiandaa kuishi bila Manji ambaye alitan­gaza kujiuzulu nafasi yake.

 

Manji aliondoka Yanga mwaka jana, lakini juzi kwenye mkutano wa wana­chama wakapinga kujiuzulu kwake wakimuomba are­jee, hapo unaweza kujiuliza kwanza kwa kipindi chote ambacho Sanga alikaimu alionyesha wazi hana uw­ezo wa kuwa mwenyekiti na ndiyo maana wanachama wakaomba Manji arejeshwe.

 

Hilo lilikuwa ‘tusi’ kubwa kwa Sanga hata kama na yeye alitaka Manji arudi kama inavyosemwa, kwa kitendo hicho pekee ki­naonyesha kuwa Sanga hakuwa akitosha kwenye viatu vya kuwa bosi mkubwa katika taasisi hiyo kubwa.

 

Achana na hayo, ndani ya muda mfupi ambao ame­kaimu uongozi, ameshindwa kuifanya klabu kuwa na umoja, makundi yamekuwa mengi na kila mtu amekuwa na nguvu ya kusema hiki na kile, kuamua hiki na kile.

Unapokuwa kiongozi wa juu kisha ukashindwa kudhibiti watu wako wa chini kufanya maamuzi kiholela na mbaya zaidi yakawa na hasara kwa taasisi, hiyo inamaanisha umeshindwa kuongoza.

 

Sanga wakati akitanga­za kujiuzulu alielezea ku­fuatwa nyumbani na watu waliokuwa na mapanga na silaha nyingine za jadi, hilo hata mimi nalipinga halikuwa sawa na nina­likemea kwa nguvu zote.

Kuna wapuuzi wachache ambao bado wanaamini ku­bishana kwa kuumizana kwa silaha ndiyo njia ya kufikisha ujumbe wakati unaweza kutumia hoja, kwa hilo li­lilotokea pole sana Sanga.

 

Sanga huyuhuyu ame­onyesha wazi kushindwa kuendesha timu, hata kama klabu siyo mtu mmoja bado hiyo haiondoi uhalisia kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka ya juu ya uongozi na anayo mamlaka ya ku­waonyesha njia wengine wa chini yake ili wamfuate.

Klabu imekuwa ikilia njaa, mikataba ya wachezaji in­aisha hakuna juhudi za kueleweka zilizokuwa ziki­fanyika, Sanga aliacha mam­bo yaende kama zile zama za zamani za kila mdau kusajili mchezaji wake, ndiyo maa­na ikaundwa ile kamati maa­lum ya kina Abbas Tarimba.

 

Tangu wiki iliyopita niliele­za kuwa sikuwa na imani na kamati hiyo na nilijua haitakuwa na mwisho mzuri kwa kuwa ilikuwa ikibeba majukumu ya watu ambao wapo kwenye uongozi na ndiyo majukumu yao, kwa asili ya soka letu nilijua ni vita, na ndicho kilichotokea.

 

Wakati yote hayo yak­iendelea kutokea Sanga alitumia muda mwingi kuwa kimya, kama alikuwa aki­fanya matukio ya uongozi basi ilikuwa ni ya ndani am­bayo hayana faida wakati mambo yameshakuwa mabaya hadharani.

Unapoona kuna mgogoro unafukuta au unakuwa mkubwa kwenye taasisi kisha kiongozi wa juu yupo kimya, huku kukiwa na malalamiko mengi juu yake mwisho wake huwa ni mbaya.

 

Mbali na hapo, katika picha ya kawaida tu Sanga alionye­sha hakuwa na nia ya dhati ya kuiongoza Yanga am­bayo kwa sisi watu wa soka tunajua jinsi ambavyo soka linavyoweza kuwa kama imani kwa watu, hivyo, nam­takia Sanga safari njema.

Kwa ufupi nimwambie tu hakuwa na uwezo wa kuvaa viatu vya kuwa bosi namba moja wa klabu hiyo na kujiu­zulu kwake siyo kwa bahati mbaya, ilikuwa lazima itokee.

Na Vuvuzela na John Joseph