×

MCHIMBA KABURI AFICHUA SIRI BIASHARA YA MAITI ZA WATOTO

MIONGONI mwa matukio ya kutisha ambayo ukisimuliwa lazima ushike tama ni pamoja na madai kwamba, wapo watu ambao wanafanya biashara ya kuuza viungo vya binadamu na maiti za watoto ambapo mmoja wa wachimba kaburi jijini Dar, Idrisa Haruna anayafungukia madai hayo na kuanika siri nzito.  Katika mahojiano maalum na Risasi Mchanganyiko, Idrisa aliyafungukia madai hayo kufuatia tetesi kuwa, wahusika wakuu wa kuuza viungo vya binadamu na maiti za watoto ni wachimba makaburi huku wateja wao wakubwa wakidaiwa kuwa ni wafanyabiashara, wanasiasa na waganga wa kienyeji.

Madai hayo yanashibishwa na matukio ambayo yamekuwa yakitokea maeneo mbalimbali nchini ya baadhi ya makaburi kukutwa yakiwa yamefukuliwa huku miili ikiwa imechukuliwa.

“Haya mambo yanafanyika kwa imani potofu za kishirikina, kuna baadhi ya wachimba makaburi ambao wanacheza dili na wafanyabiashara na wanasiasa, wengine wanataka viungo vya binadamu na wengine kwenda mbali zaidi na kuhitaji maiti za watoto wadogo, huoni hii ni hatari?

“Yaani leo hii unamzika mwanao, unaondoka, kesho unakuta kaburi limefukuliwa au wanafukua halafu wanafukia, wewe unajua mati ya mwanao ipo kaburini kumbe watu wameshafanya mambo yao,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Kessy anayeishi karibu na makaburi yaliyopo maeneo ya Mbagala jijini Dar.

MCHIMBA KABURI  HUYU HAPA

Kufuatia madai hayo, waandishi wetu walifanya jitihada za kuzungumza na Idrisa anayefanya shughuli zake za uchimbaji wa makaburi maeneo ya Tandika jijini Dar ambaye alianika siri nzito. “Nina umri wa miaka 33, tulianza kuchimba makaburi kama sadaka kwa sababu katika Dini ya Kiislam ni kazi ambayo mtu yeyote anapaswa kuifanya kwa ajili ya kuhifadhi wenzetu waliotangulia mbele za haki.

“Mimi nimejifunza kazi hii kipindi ambacho wazazi wetu walikuwa wakiifanya kama kujitolea, nikawa naenda nao na kuangalia kile wanachokifanya, mwishowe tumekuwa watu wazima na sisi tunaifanya kazi hii,” alieleza Idrisa na kuendelea:

BIASHARA YA MAITI VIPI?

“Hiyo ni kati ya changamoto kubwa sana tunayokutana nayo. Unaweza kukuta mtu anakuja na kukuambia anahitaji mizizi ya chini kwenye kaburi, au anakuambia anataka viungo f’lani na wengine wanakuambia wanataka maiti za watoto wadogo.

“Ujue tunapochimba kaburi wakati mwingine huwa tunakutana na viungo vya binadamu kama vile mkono, kichwa au fuvu, mguu na sehemu nyinginezo, tunachofanya ni kuchukua viungo hivyo na kwenda kuvifukia kwingine. “Kwa imani yangu wanaokuja ili niwauzie viungo vya binadamu huwa nawakatalia, najua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria pia.

“Wengi wao wanakuja katika vipindi vya uchaguzi, wanaokuja ni wapambe wa viongozi, wanakuambia wanataka vitu hivyo. Unabaki kujiuliza wanakwenda kufanyia nini? Lakini mwisho unaona tu ni mambo ya kishirikina ambayo hayana msingi.”

MATEJA NDIYO

MADILI YAO

Hata hivyo, licha ya Idrisa kukiri kufuatwa na watu wengi wakitaka wafanye biashara hiyo haramu, lakini kutokubaliana nao, gazeti hili lilifanya uchunguzi na kubaini kuwa, wanaoifanya biashara hiyo ni wale wachimbaji wa kaburi ambao ni watumiaji wa madawa ya kulevya ‘mateja’.

Mmoja wa wachimba kaburi maeneo ya Sinza-Makaburini jijini Dar aliyejitambulisha kwa jina Sadick alisema: “Unajua sisi kazi yetu ni kuchimba kaburi, sasa siku nyingine wakati tunachimba inaweza kuwa sehemu hiyo alishazikwa mtu siku za nyuma kidogo, tukikutana na mifupa, tunaiweka kando tu.

“Sasa akija mtu akasema anataka fuvu kwa mfano, kidilidili mtu aliyefyatuka anaweza kuuza, si unajua tena ukishatajiwa pesa? “Lakini wengi wanaofanya biashara ya kuuza viungo vya binadamu na hizo maiti za watoto ni mateja, wale hawajali. Ukishawatajia pesa wanapagawa kabisa,” alisema Sadick.

GHARAMA ZA UCHIMBAJI

Akizungumza na mwandishi wetu, Idrisa alisema kuwa, mara nyingi mtu anapofiwa akienda kwao kwa ajili ya kuchimbiwa kaburi, hawapatani bei.

“Tuko timu ya watu sita, akija mtu akataka huduma ya kuchimbiwa kaburi, hatumtajii gharama, sisi tunachimba halafu yeye mwenyewe anaangalia atatupa shilingi ngapi, mara nyingi ni kuanzia shilingi elfu 30 kwenda juu,” alisema Idrisa.

KUTOKA RISASI

Kufanya biashara ya kuuza viungo vya binadamu ni kosa kisheria, lakini hata kibinadamu si kitu kizuri hivyo tunawatahadharisha wanaojipatia pesa kwa njia hiyo waache mara moja kabla ya hayajawafika makubwa