×

DIANA KIMARI ADAIWA KUKACHA KANISA!

Image result for Diana Kimari
Diana Kimari

UBUYU ukimpa asiye na meno, kamwe hawezi kumung’unya, raha yake mpe mwenye meno yote 32! Ubuyu uliotua kwenye meza ya Ijumaa Wikienda wiki hii unamgusa mwigizaji mdogo na machachari, Diana Kimari. Diana anadaiwa kulikacha kanisa alilokuwa akisali awali la Nabii Mwamposa lililopo Mwenge jijini Dar. Mwigizaji huyo anadaiwa kukacha baada ya kuibuka kwa skendo kuwa anatoka na mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo (jina linahifadhiwa kwa sasa).

Kwa mujibu wa msambaza ubuyu wetu, habari za staa huyo wa filamu zilianza kusambaa kanisani hapo kwa waumini mbalimbali na hata wa nje ya kanisa hilo, jambo ambalo lilikuwa chukizo kubwa kwa Diana na kuamua kukata mguu kidogokidogo hadi akapotea kabisa, pamoja na kwamba alikuwa mhudhuriaji mzuri wa kanisa hilo.

CHANZO CHATIRIRIKA

“Unajua Diana alikuwa mstari wa mbele kanisa hapo kwani alikuwa akijituma sana kwenye shughuli za utumishi na alikuwa karibu sana na mchungaji huyo, lakini baadaye kukazuka manenomaneno kanisani hapo kuwa anatoka kimapenzi na mtumishi huyo wa Mungu.

“Kufuatia ishu hiyo, ndipo Diana akaamua kukata kabisa mguu kufika kanisani,” kilidai chanzo hicho.

IJUMAA WIKIENDA SASA

Baada ya kupata ubuyu huo, Ijumaa Wikienda lilifanya kama kawaida yake ambapo lilimtafuta Diana ili kuthibitisha madai hayo ambapo aliamua kuweka wazi kila kitu kuhusiana na sekeseke hilo kama ifuatavyo;

Ijumaa Wikienda: Mambo vipi Diana? Nasikia kuwa kanisa ulilokuwa unasali umefukuzwa au umekacha na siku hizi huonekani, hili likoje?

Diana: Kwanza ngoja niliweke wazi hili jambo. Ieleweke kwamba mimi sijawahi kufukuzwa kanisani kama wanavyosema, bali niliamua mwenyewe kuhama na kusali kanisa lingine.

Ijumaa Wikienda: Je, ni kitu gani kilikufanya ukahama hilo kanisa sasa?

Diana: Unajua pale kulizuka maneno mengi sana ya kuwa mimi natembea na mchungaji, jambo ambalo sikulipenda, ndipo nikaamua kuhama hapo kanisani.Image result for Diana Kimari

Ijumaa Wikienda: Kwa nini sasa waliamua kukusingizia wewe?

Diana: Unajua mtu anaweza kukuona msichana mdogo labda akajua una mafanikio au ukivaa ukapendeza watu wanakuchukulia tofauti na kingine nafikiri ni wivu tu.

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo sasa hivi unasali wapi?

Diana: Hiyo ni siri yangu ila nimetoka pale (Kwa Mwamposa) kwa sababu ya manenomaneno ambayo siyataki kabisa, sasa hivi ninataka amani tu moyoni mwangu.

Ijumaa Wikienda: Nashukuru kwa ushirikiano wako Diana.

Diana: Asante sana karibu tena.

KANISA LINASEMAJE?

Hata hivyo, jitihada za Ijumaa Wikienda kuufikia uongozi wa kanisa hilo na mchungaji aliyehusishwa na Diana ziligonga mwamba baada kuzuiwa na walinzi kuingia kwenye kanisa hilo.

SKENDO YAIBULIWA

Miezi kadhaa iliyopita gazeti hili lilipokea skendo hiyo ya Diana kutembea na mchungaji kutoka kwa mmoja wa waumini ambapo lilimtafuta mrembo huyo akawa anachenga, lakini sasa amepatikana na kueleza ukweli wake.

MAKALA: Imelda Mtema, DAR