×

Watoto warekebishwa uti wa mgongo kabla ya kuzaliwa

surgery

MADAKATARI nchini Uingereza wamerekebisha uti wa mgongo wa watoto wawili wiki kadhaa kabla ya kuzaliwa.

Oparesheni hiyo ya kwanza ya kipekee nchini humo ilifanywa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha London mwaka huu wakati watoto hao wakingali tumboni mwa mama yao.

 

Watoto hao walikuwa wamekumbwa na tatizo liitwalo ‘spina bifida’ ambalo hutokea wakati wa ujauzito ambapo mifupa ya uti wa mgongo haikui kwa kawaida, hivyo kuacha nafasi ambayo huuacha uti huo ukiwa hauna kinga dhidi ya mitikisiko.

 

Hitilafu hiyo inaweza kusababisha  ute wa uti huo kuvuja na hivyo kuhatarisha ubongo.  Kasoro hiyo kwa kawaida hutibiwa baada ya kuzaliwa lakini utafiti unaonyesha tiba hiyo ya mwanzo inaweza kuzuia kuvuja kwa ute huo na kumfanya mtoto awe na afya njema na kutembea bila matatizo.

Wanawake wajawazito wa Uingereza, awali walilazimika kwenda Marekani, Ubelgiji na Switzerland kwa tiba hiyo ambayo huchukua dakika 90 na yenye hatari ya kuanzisha uchungu wa kuzaa kabla ya muda wake kufika.