SERIKALI ya Rwanda imevitaka vyama vya michezo nchini humo kusimamisha ratiba zote za kimichezo ambazo zinaitaka Rwanda kwenda kushiriki nje ya nchi hiyo hasa katika nchi zenye maambukizi ya virusi vya Corona.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na hofu ya maambukizi ya Corona na Rwanda ikiwa moja ya nchi ambazo zinafanya jitihada kuhakikisha hakuna maambukizi na hata yatakapotokea yanadhibitiwa mara moja.
Waziri wa Michezo na Utamaduni wa Rwanda, Julienne Uwacu, amevitaka vyama hivyo kuandika barua mara moja kwa Shirikisho ka Soka Barani Afrika (CAF) za kuelezea azma na sababu ya wao kutoshiriki katika michezo inayofanyika nje ya nchi hiyo.
Rwanda kwenye michezo ya kimataifa ipo katika michuano ya kufuzu AFCON mwaka 2020 ambapo katika mchezo wa mapema ilitakiwa kucheza na Uganda Aprili 6, 2020 ikiwa KUNDI C, michuano ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2022 na michuano ya CHAN 2020.
Mlipuko wa virusi vya Corona ambao uliripotiwa kwanza nchini China kuanzia Desemba mwaka jana umekuwa tishio ulimwenguni kote na umeathiri vibaya michezo ya kimataifa.
