



BENKI ya Barclays Tanzania kupitia kampeni yake ya ‘Fanya Miamala na Ushinde’ imemkabidhi Darius Tebuka, mkazi wa Dar es Salaam, TV ya kisasa (flat screen) baada ya kuibuka mshindi wa awamu ya pili kwa kufanya miamala ya kifedha kupitia huduma za kidijitali.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo, Posta jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Barclays, Joe Bendera amesema kuwa kampeni inafanyika kwa muda wa miezi mitatu ambapo mshindi wa awamu ya kwanza alishapatikana na kukabidhiwa zawadi yake na ilikuwa ni zamu ya mshindi wa awamu ya pili.
Bendera ameeleza kuwa Benki ya Barclays itaendelea kuwa karibu na wateja wake wote wanaotumia mifumo ya kidijitali kufanya miamala katika malipo ya huduma na bidhaa mbalimbali.
“Tunawaomba Watanzania wote waendelee kutuunga mkono, watumie application yetu na huduma zetu nyingine za kidijitali kufanya miamala na kulipia huduma mbalimbali kwa njia ya kidijitali kama kununua luku, kulipia bidhaa, bili za maji na huduma nyingine ili kurahisisha maisha na kuokoa muda,” alisema.
Kwa upande wake, Darius Tebuka ameipongeza benki hiyo kwa kuanzisha kampeni hiyo kwani imemuwezesha kujinyakulia TV ya kisasa na kuwataka Watanzania kuendelea kuiamini benki hiyo na kutumia mifumo ya kidijitali ya benki hiyo kufanya miamala mbalimbali.