WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe amelielekeza Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini kumchukulia hatua Msanii Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya’ kwa kumdhihaki aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba ambaye alifariki jana nchini Afrika Kusini.
Mwakyembe ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha maafusa utamaduni nchini ambapo amesema kitendo hicho kilicho fanywa na msanii huyo nikinyume na maada na tamaduni za kitanzania hivyo akamatwe na kushughuliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Dudu Baya amemjibu waziri huyo na kusema asisumbuke kuwaagiza polisi wamsake kwani watapoteza mafuta bure, badala yake wamuelekeze ni kituo gani cha polisi akaripoti.
MWAKYEMBE Amvaa DUDU BAYA “Ni Mpuuzi, Rais Ameshtuka, Akamatwe Haraka”
“Nipo nyumbani, Mheshimiwa Mwakyembe umeagiza polisi kunitafuta, usisumbue difenda kumaliza mafuta, bora wakakamte majambazi, niambie polisi waniite kituo gani, nipo tayari kufika hapo,” amesema Dudu Baya.
Hata hivyo, Watanzania wengi ambao kwa sasa wapo kwenye majonzi mazito, wamechukizwa na kitendo cha Dudu Baya kumdhihaki Ruge tena hadharani kwenye mitandao ya kijamii ilihali hatupo naye tena badala ya kumuombea apumzike kwa amani.
Pia, wamedai kupitia mitandao ya kijamii amekuwa akitumia maneno kwa kuandika, kujirekodi video na kuzisambaza kumshashifu Ruge huku akimtaja Mwenyezi Mungu kinyume na matendo ambayo anayafanya.