CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemuomba Rais wa Jamuhuri yaMmuungano wa Tanzania, Dk John Magufuli kukutana na wadau wa korosho ili aweze kufahamu changamoto wanazokutana nazo wakulima na wanunuzi wa zao hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, CECIL MWAMBE amesema wao kama chama na wadau wa zao la korosho wapo tayari kutoa ushirikiano ili wakulima waweze kunufaika na zao hilo.
Aidha, Mwambe ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuiteuwa bodi mpya ya korosho ili iweze kutekeleza majukumu yake kwani hiyo ni sheria kwa mujibu wa bunge na bado haijafutwa huku akiongeza kuwa zao la korosho ni moja kati ya mazao yanayoingiza fedha za kigeni nchini.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalum kinondoni na waziri kivuli wa elimu SUZAN LYIMO amesema kuwa watoto wengi wanaoanza kidato cha kwanza wemeshindwa kuanza masomo yao kutokana na wazazi wao kutolipwa fedha zao za korosho, ambapo ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuwalipa fedha zao wakulima hao ili kutatua changamoto za elimu katika mikoa ya kusini.
Sakata hilo la zao la korosho lilianza kuchukua sura mpya baada wafanyabiasha kutaka kununua korosho hizo kwa bei ya shilingi 1,900 mpaka 2,700 kwa kilo moja ambapo Serikali ikaagiza zao hilo linunuliwe kwa shilingi 3,300 kwa kilo.