×

MADEE UKOROFI WAZIDI, APELEKWA KWA BIBI YAKE

BAADA ya kumaliza simulizi ya Mboto, Kilinge leo inaanza kuangalia maisha yote ya msanii maarufu wa muziki wa Kizazi Kipya, Hamadi Ally Sheneda au maarufu kwa jina la Madee. Kwa kuanza tu naomba nikufahamishe kwamba, Madee kama wengi mnavyomfahamu ni kwamba jina hilo alipewa na muandaaji wa muzki hapa nchini, Paul Matthysse ‘P-Funk.

 

Majani’, baada ya kwenda studio kwake kurekodi wimbo uliompa umaarufu, uliofahamika kwa jina la Kazi ya Mola.

 

Sasa endelea kumsikia mwenyewe akielezea maisha yake kwa ujumla.

MIMI ni mzaliwa wa Dar es Salaam, ila baba yangu na mama yangu walibahatika kupata watoto watano, wa kwanza alikuwa anaitwa Ally ila bahati mbaya ameshatangulia mbele za haki, walifuata mapacha wanaitwa Adam na Abdallah na baada ya hao nilifuata mimi na wao wanaendelea na maisha yao na wa mwisho ni dada yangu ambaye anaitwa Chonge kama nilivyoamua kumuita mwanangu.

 

“Kwa ufupi tu ni kwamba mwanangu Chonge nimeamua kumuita jina hilo kwa sababu ninampenda sana mdogo wangu Chonge kwa kuwa ndiye kitinda mimba wetu, niliamua kumuita hivyo ili nibadili ile dhana ya wengi waliokuwa wamezoea eti mtoto ni lazima aitwe jina la babu yake, kwani hata ukian­galia mtoto wangu wa kwanza Saida hata yeye jina hilo ni la dada yangu, mtoto wa mama yangu mdogo.

 

“Lakini kama unakumbuka pia utaona kuna wimbo wa MB Dog alinishirikisha mwaka 2006, ulikuwa unaitwa Ina Maana, humo ndani nilikuwa namsifia dada yangu Saida, ingawa lengo la wimbo huo MB Dog alikuwa akimsifia Nancy Sumari lakini kutokana na mapenzi yangu kwa dada zangu, nikaona nitumie fursa hiyo kumsifia dada yangu.

 

“Nadha­ni hii ndiyo itakuwa system ya maisha yangu, hasa kwa wa­toto wangu kwani kila ni­takayem­zaa mimi nitamuita jina la kaka zangu au dada zangu ili nibadilishe tu ile hali ambayo wengi wamekuwa wakidhani kuwa kumuita mwanao jina na mzazi wako ndiyo sheria.

 

“Kwa kifupi, nikirudia katika maisha yangu ya utotoni, naomba watu wajue tu kuwa Madee nilikuwa ni mtoto mkorofi na mtukutu sana kiasi kwamba wazazi wangu walikuwa hawaishi kupata kesi juu yangu hapo mtaa­ni kwetu Manzese jijini Dar es Salaam.

 

“Nakumbuka mara baada ya kuanza tu darasa la kwanza, nilifanya vurugu nyingi sana kwa wanafunzi wenzangu kiasi kwamba wazazi wangu wakawa ha­waishi kuletewa kesi jambo ambalo baba alishindwa kulivumilia na kuamua ku­nihamishia Tanga kwa bibi yangu, yaani mama yake baba.

 

“Walinihamishia katika Shule ya Msingi Kisima Tui, shule hiyo ipo Kata ya Pongwe iliyopo Tanga mjini. Walinipeleka kwa bibi kutokana na kumuamini kwa malezi yake kwani alikuwa akisifika kwa ukali, yaani alikuwa mkali sana, hivyo baada ya kwenda kule kweli siku za mwanzo nilibadilika sana maana hakuwa na mchezo kabisa.

 

“Maisha yangu ya shule yaliendelea kwa aina hiyo lakini baada ya kufika darasa la pili nakumbuka mara tu nilipozoea maz­ingira ya shule, tulianza mtindo wa kutoroka ule muda tu wa mapumziko na kwenda katika shamba moja lilikuwa linaitwa Mtovivi, hilo shamba lilikuwa linasifika sana kwa Mafenesi hivyo tulikuwa tunaenda kuiba na baadaye muda wa kurudi nyumbani tunayachukua na kwenda nayo nyumbani.

 

“Ujue bibi yangu huyo ni Mdigo, hivyo hata kabila la baba yangu ni Mdigo kabisa wa kutoka Tanga, hivyo kila tulipokuwa tunarudi nyumbani, bibi alikuwa anashangaa kila siku nikifika naingia na Mafenesi ila ka­diri siku zilivyokuwa zinaen­da kuna siku moja tulienda kule yule mama mwenye shamba hilo alitufuma sema tukakimbia hakutushika, in­gawa aliamua kwenda hadi shuleni na kuwaambia wal­imu kuwa kuna wanafunzi sijawakariri wana tabia ya kuiba mafenesi yangu.

 

“Hivyo ailitoka pale amewapa tahadhari na aki­waambia kabisa wawaonye wanafunzi la sivyo siku akiwakamata kitakachowa­tokea wasimlaumu kwa lol­ote maana alikuwa akifuga mbwa wa hatari, baada ya kusikia taarifa hizo, tuli­pumzika kwenda kuiba kwa wiki moja, baadaye tulianza tena.

 

“Siku moja ilipopigwa kengele ya mapumziko tu tuliondoka na rafiki zangu wawili, mmoja alikuwa akiitwa Stephano au Sity mwingine alikuwa anaitwa Chikantu, siku hiyo tu­meenda moja kwa moja hadi shambani baada ya kufika tu kumbe mlinzi ametuona, akafungulia mbwa,” anase­ma Madee.

Je, baada ya mlinzi ku­fungulia mbwa nini kilito­kea? Tukutane wiki ijayo. 0715332033.