VITA nzito ya kujibizana kwa maneno imeibuka kati ya Mchungaji wa Kanisa la Maombezi la GRC lililopo Ubungo- Kibangu jijini Dar, Anthony Lusekelo almaarufu Mzee wa Upako na Mchungaji wa Mitume na Manabii, Daudi Mashimo, Risasi Jumamosi lina ishu kamili.
MASHIMO AIBUKA
Vita hiyo imeibuka hivi karibuni baada ya Mchungaji Mashimo kuibuka na kuwatolea unabii wa mambo mbalimbali wachungaji wenzake akiwemo Mzee wa Upako akidai kuwa kuna roho wa mauti anamzunguka mtumishi huyo wa Mungu.
UZUSHI
Hivi karibuni ilizagaa taarifa ya kizushi kuwa Mzee wa Upako amefariki dunia baada ya kudhoofu mwili, taarifa ambayo mwenyewe aliipokea kwa masikitiko na kuishia kuwajibu kama alivyowahi kusema Yesu Kristo kwa wabaya wake: “Baba uwasamehe kwa maana hawajui watendalo.”
BINTIYE AFUNGUKA
Katika mahojiano na gazeti ndugu la hili, Ijumaa lililoingia mtaani jana, binti wa Mzee wa Upako, Salome Anthony Lusekelo alieleza kuwa, baba yake alisikia taarifa za Mashimo kudai kuoneshwa unabii na kumtaka ajiombee kwanza mwenyewe na kuacha kutafuta umaarufu kupitia jina la baba yake.
Baada ya majibu hayo ya Mzee wa Upako ilikuwa ni kama ameshamalizana na wabaya wake, lakini katika kuonesha yuko kwenye vita nyingine juzi (Alhamisi) Mchungaji Mashimo aliibuka na kumwambia Mzee wa Upako kuwa unabii wa kifo chake uko palepale.
MASHIMO AITA WANAHABARI
Akizungumza na wanahabari juzi, Mchungaji Mashimo alisema ameoteshwa ndoto ya kinabii juu ya Mzee wa Upako katika kipindi cha mwezi wa nne, tano na wa sita kuwa atapitia katika wakati mgumu sana asipofanya sala ya toba.
“Yaani ndugu wanahabari nawaambia Mchungaji Anthony Lusekelo kama asipofanya toba, ikifika mwezi wa sita atakuwa na hali mbaya mno.
“Huo ndiyo ushauri ninaompa, akitaka aufanyie kazi, akitaka aupuuzie, lakini hilo ndilo nililooteshwa kinabii na lazima likamilike kama hatafuata ushauri wangu.
“Baada ya kuoteshwa hivyo, nilikwenda mpaka kanisani kwa Mzee wa Upako, Ubungo-Kibangu nikamkosa na kuishia kupewa namba yake, lakini hata hivyo, nilipomtafuta kwa njia ya simu pia sikufanikiwa kumpata.
“Sasa alipozushiwa kifo badala ya kufanya sala ya toba yeye anaibuka na kujitapa eti yuko juu na atabaki kileleni, hiyo ni kumkufuru Mungu.
“Hivyo kupitia vyombo vya habari, naamini ujumbe utamfikia na kufanya nilivyomwagiza na kama akidharau, basi Mungu ambariki,” Mchungaji Mashimo alimalizia.
Kufuatia msisitizo wa Mchungaji Mashimo juu ya unabii huo, mwanahabari wetu alimpigia simu Mzee wa Upako, lakini simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.
“SIFI LEO WALA KESHO”
Chanzo cha taarifa juu ya afya ya Mzee wa Upako ni picha iliyosambaa mitandaoni wiki iliyopita ambayo ilimuonesha akiwa amedhoofu na kwamba ni mgonjwa, jambo ambalo amelikanusha mwenyewe akisema: “Sifi leo wala kesho.”
Hata hivyo, katika mkutano wake na wanahabari, Mchungaji Mashimo aliendelea kusisitiza kuwa Mzee wa Upako asipotubu, atakufa hivi karibuni, jambo ambalo linakinzana na vitabu vitakatifu vya Mungu kwa maana mwamuzi wa kifo ni Mungu mwenyewe na wala siyo binadamu awaye yote.
MASHIMO AVALIWA NJUGA
Hata hivyo, kufuatia Mchungaji Mashimo kutoa unabii wa mambo mbalimbali mara kwa mara, hivi karibuni watu mbalimbali walimvalia njuga na kumwambia aache kutafuta kiki kupitia majina ya watu.
STORI: Richard Bukos, Risasi Jumamosi