
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Waislamu wote nchini watumie siku kuu ya Eid el Fitr kwa kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.
Ameyasema hayo wakati aliposhiriki swala ya Eid El Fitr katika msikiti wa Anwar uliopo Msasani jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kwamba wakati huu ni mzuri kwa kuimarisha mshikamano miongoni mwa Watanzania wa madhehebu mbalimbali ambapo amewakumbusha wazazi na walezi kuwaongoza watoto kwa kuwapa mafundisho ya dini yatakayowawezesha kumjua Mwenyezi Mungu na kuwa raia wema.
Awali, imamu wa msikiti huo, Sheikh Mhina, alisema Waislamu wanatakiwa kuitumia siku ya leo kwa kuhamasisha amani pamoja na kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo na kuyaendeleza mema yote waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.